SIRRO ATAKA MADIWANI WAIKATAE MIRADI ISIYO NA VIWANGO
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma Balozi Simon Sirro amewataka madiwani mkoani Kigoma kutokuwa sehemu ya utekelezaji wa mirai au miradi isiyokamilika badala yake wasimamie kwa karibu na kuhakikisha miradi inakamilika na kuleta maendeleo kwa wananchi.
Balozi Sirro amesema hayo katika Mkutano wa Baraza Maalum la Madiwani la kujadili hoja na mapendekezo ya Mdhibiti na Mkaguzi Mkuu wa Hesabu za Serikali (CAG) Wilaya ya Uvinza Mkoani Kigoma na kubainisha kuwa madiwani kama wawakilishi wa wananchi wanapaswa kuwa wakali kuhakikisha miradi inakamilika kwa wakati na kuwa na viwango vinavyokubalika.
Mkuu huyo wa mkoa alisema kuwa ni jambo la kushangaza inapotokea Mradi unatekelezwa chini ya kiwango wakati Mwakilishi wa wananchi yupo katika eneo hilo na kushindwa kuchukua hatua zozote na kusababisha malalamiko kwa Serikali.
Sambamba na hilo Balozi Sirro amewakumbusha Madiwani na wataalam katika Halmashauri za mkoa Kigoma kusimamia ukusanyaji wa mapato na pamoja na kuchukua hatua kwa mtumishi au kiongozi yeyote atakayebainika kufanya ubadhilifu kupitia makusanyo hayo.
Mkuu wa Mkoa wa Kigoma, Balozi Simon Sirro, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Uvinza kwa kupata hati safi katika ukaguzi wa hesabu za Serikali kwa mwaka wa fedha 2024/2025 pamoja na kupunguza idadi ya hoja za ukaguzi, hatua inayoashiria kuimarika kwa usimamizi wa fedha za umma na uwajibikaji katika utekelezaji wa majukumu.
Kwa upande wake, Mkuu wa Wilaya ya Uvinza, Dinah Mathamani, amesema kuwa ofisi yake imeendelea kusimamia kwa karibu utendaji wa halmashauri hasa kwenye suala la mapato na matumizi na kuwezesha Halmashauri kuchukua hatua za kurekebisha mapungufu yaliyobainishwa na ukaguzi wa CAG.
Mkuu huyo wa Wilaya alisema kuwa ofisi yake inaendelea kufuatilia kwa karibu kuhakikisha hoja zilizobaki zinapatiwa ufumbuzi kwa wakati lakini pia kuwepo na nidhamu ya matumizi ya halmashauri na utekelezaji wa miradi unaozingatia ubora.



