Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MIKOPO NAFUU YA VITUO VYA MAFUTA VIJIJINI, MATUMANI KWA WANANCHI

MIKOPO NAFUU YA VITUO VYA MAFUTA VIJIJINI, MATUMANI KWA WANANCHI

 



Na Matukio DaimaMedia 


Kwa muda mrefu, wananchi wa maeneo mengi ya vijijini wamekuwa wakikabiliwa na changamoto ya upatikanaji wa mafuta ya petroli na dizeli, wengine wamekuwa wakisafiri kilomita nyingi kufuata huduma hiyo, huku wengine wakitegemea wauzaji wasiokuwa rasmi wanaouza mafuta kwenye chupa za plastiki, madumu na vyombo vingine visivyokidhi viwango vya usalama.


Changamoto hiyo ndiyo iliyoipelekea Serikali kupitia Wakala wa Nishati Vijijini (REA), kwa kushirikiana na Benki ya Azania, kuzindua mpango wa utoaji wa mikopo nafuu kwa ajili ya ujenzi wa vituo vidogo vya mafuta vijijini, Mplango huo unalenga kusogeza huduma za mafuta karibu na wananchi, kuongeza usalama wa matumizi ya nishati na kufungua fursa mpya za maendeleo ya kiuchumi katika maeneo ambayo kwa muda mrefu yamekuwa nyuma katika uwekezaji wa huduma za mafuta.


Akizungumza wakati wa uzinduzi wa mpango huo, Katibu Mkuu wa Wizara ya Nishati anayeshughulikia Mafuta na Gesi, Dkt. James Mataragio, alisema mafuta ni nguzo muhimu ya maendeleo ya uchumi na ustawi wa jamii. Alieleza kuwa Serikali imeamua kuanzisha mpango huo ili kupunguza tofauti kubwa ya bei ya mafuta kati ya mijini na vijijini pamoja na kuondoa adha ya wananchi kusafiri umbali mrefu kufuata huduma hiyo.


Kwa mujibu wa Dkt. Mataragio, hatua hiyo pia ni suluhisho la kudumu kwa biashara hatarishi ya kuuza mafuta katika vyombo visivyo salama, alibainisha kuwa ujenzi wa vituo vinavyokidhi viwango vya kitaifa utapunguza ajali za moto, kulinda maisha ya wananchi na kuhakikisha biashara ya mafuta inafanyika katika mazingira salama na yanayosimamiwa na sheria.



Mhandisi Hassan Saidy, ni Mkurugenzi wa Wakala wa Nishati Vijijini (REA),  alisema baada ya mafanikio makubwa ya kupeleka umeme vijijini, Serikali imeona ni wakati wa kupanua huduma nyingine za nishati kwa kuhakikisha mafuta yanapatikana kwa urahisi katika maeneo ambayo kwa muda mrefu hayakuvutia wawekezaji kutokana na changamoto za kibiashara.


Kwa mujibu wa Mhandisi Saidy, kukosekana kwa vituo rasmi vya mafuta kumewalazimu wananchi kununua mafuta kwa gharama kubwa na wakati mwingine kutoka kwa wauzaji wasiokuwa rasmi, hali hiyo imeongeza gharama za uzalishaji kwa wakulima, wafugaji, wavuvi na wafanyabiashara, huku pia ikidhoofisha kasi ya maendeleo ya uchumi wa maeneo ya vijijini.


Ili kuhakikisha mpango huo unatekelezwa kwa mafanikio, Mkurugenzi wa Nishati Jadidifu na Teknolojia za Nishati Mbadala kutoka REA, Mhandisi Advera Mwijage, alisema Serikali imetenga zaidi ya shilingi bilioni 12 kwa ajili ya utekelezaji wa mradi huo kote nchini, alieleza kuwa ndani ya miaka mitatu iliyopita REA imepokea maombi 258 kutoka kwa wawekezaji mbalimbali, lakini wanufaika wanane ndio waliokamilisha masharti na kusaini mikataba ya mikopo yenye thamani ya zaidi ya shilingi bilioni moja.


Kwa mujibu wa Mhandisi Mwijage, idadi hiyo ni mwanzo tu wa utekelezaji wa mradi, kwani maombi mengine yanaendelea kufanyiwa tathmini huku Serikali ikiendelea kuhamasisha wawekezaji zaidi kushiriki katika mpango huo.


Hata hivyo, mafanikio ya mradi hayategemei upatikanaji wa fedha pekee, bali pia usimamizi mzuri wa uwekezaji.


Mkurugenzi wa Maendeleo ya Biashara wa Benki ya Azania, Yahya Mbanka, alisema benki hiyo imejipanga kuhakikisha mikopo yote inasimamiwa kwa uwazi na ufanisi,  alifafanua kuwa pamoja na kutoa fedha, benki itawapatia wanufaika elimu ya fedha, ushauri wa biashara na ufuatiliaji wa karibu ili kuhakikisha miradi hiyo inakuwa endelevu na inaleta matokeo yaliyokusudiwa.


Mbanka alisema hatua hiyo itasaidia kujenga biashara imara zitakazoongeza ajira, kuchochea uwekezaji na kuinua uchumi wa maeneo ya vijijini kwa muda mrefu.



Kwa upande wa wanufaika, Boaz Nyakeke, ambaye ni mmoja wa waliopata mkopo katika awamu ya kwanza, alisema mpango huo utakuwa mkombozi kwa wananchi wengi wa vijijini, alieleza kuwa vituo hivyo vitarahisisha upatikanaji wa mafuta kwa bei zinazozingatia miongozo ya Mamlaka ya Udhibiti wa Huduma za Nishati na Maji (EWURA), hatua itakayowanufaisha wakulima, wavuvi, wasafirishaji na wafanyabiashara wengine wanaotegemea mafuta katika shughuli zao za kila siku.


Kwa ujumla, uzinduzi wa mpango huu unaashiria hatua mpya katika safari ya Serikali ya kuimarisha upatikanaji wa huduma za nishati nchini, baada ya mafanikio ya miradi ya umeme vijijini, sasa Serikali imeelekeza nguvu katika kuhakikisha huduma za mafuta nazo zinawafikia wananchi wa pembezoni kwa usalama, urahisi na gharama nafuu.


Iwapo utekelezaji wa mpango huu utaendelea kwa kasi iliyopangwa, Tanzania inaweza kushuhudia kupungua kwa biashara holela ya mafuta, kuongezeka kwa ajira na uwekezaji, pamoja na kukua kwa uchumi wa vijijini, hivyo, mradi huu si wa kujenga vituo vya mafuta pekee, bali ni uwekezaji wa kimkakati unaolenga kubadilisha maisha ya wananchi na kuifanya nishati kuwa chachu ya maendeleo jumuishi nchini.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3