MHUDUMU WA MISAADA WA UINGEREZA YUKO CHINI YA UANGALIZI KWA HOFU YA EBOLA KATIKA HOSPITALI YA LONDON
Mhudumu wa misaada ya kibinadamu kutoka Jamhuri ya Kidemokrasia ya Congo amehamishiwa nchini Uingereza kwa uangalizi wa kitabibu baada ya uwezekano wa kuathiriwa na virusi vya Ebola akiwa kazini.
Shirika la Usalama wa Afya la Uingereza (UKHSA) limesema mtu huyo, ambaye ni mkazi wa Uingereza na jina lake halijawekwa wazi, hana dalili zozote za Ebola kwa sasa, na hatua ya kumhamisha imechukuliwa kama tahadhari.
Kwa mujibu wa UKHSA, mhudumu huyo anaendelea kuwa katika hali nzuri kiafya lakini anafanyiwa vipimo na kufuatiliwa katika hospitali moja jijini London.
Jina la hospitali hiyo halijatangazwa, ingawa Hospitali ya Royal Free kaskazini mwa London ina kitengo maalumu cha kuwahudumia wagonjwa wenye magonjwa hatari ya kuambukiza.
Kipindi cha kujitokeza kwa dalili za Ebola ni kati ya siku mbili hadi 21, hivyo mhudumu huyo atalazimika kujitenga kwa muda wote wa kipindi hicho.
Mhusika huyo alikuwa akifanya kazi na shirika la misaada lililokuwa likisaidia kukabiliana na mlipuko wa Ebola nchini DRC.
Ebola ni ugonjwa hatari sana unaosababishwa na virusi. Tofauti na mafua au Covid-19, virusi vya Ebola haviambukizwi kwa njia ya hewa, bali huenea kupitia kugusana moja kwa moja na majimaji ya mwili wa mtu aliyeambukizwa.
Dalili zake huanza ghafla na zinafanana na za mafua au malaria, zikiwemo homa, maumivu ya kichwa na uchovu.
Ugonjwa unapoendelea, mgonjwa anaweza kutapika, kuharisha na kushindwa kwa baadhi ya viungo vya mwili kufanya kazi. Baadhi ya wagonjwa pia hutokwa na damu ndani na nje ya mwili.
Richard Pebody, Mkurugenzi wa Kitengo cha Magonjwa ya Mlipuko na yanayoibuka katika Shirika la Usalama wa Afya la Uingereza (UKHSA), amesema:
"Hatari kwa umma kwa ujumla bado ni ndogo. Mtu huyu amehamishwa kama hatua ya tahadhari ya ziada, na tunafurahi kuwa anaendelea kuwa katika hali nzuri."
UKHSA pia imesema kwa sasa hakuna kesi yoyote iliyothibitishwa ya ugonjwa wa Ebola nchini Uingereza.