Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MBUNGE MASACHE: UPATIKANAJI WA MAJI CHUNYA WAPANDA KUTOKA ASILIMIA 26 HADI 52

MBUNGE MASACHE: UPATIKANAJI WA MAJI CHUNYA WAPANDA KUTOKA ASILIMIA 26 HADI 52

 


Na Matukio Daima Media, Chunya

MBUNGE wa Jimbo la Lupa wilayani Chunya, mkoani Mbeya, Masache Kasaka, amesema upatikanaji wa maji katika jimbo hilo umeongezeka kutoka asilimia 26 mwaka 2020 hadi kufikia asilimia 52 kwa sasa, tangu alipochaguliwa kuwa mwakilishi wa wananchi.


Hata hivyo, amesema pamoja na mafanikio hayo, bado kuna changamoto kubwa ya upatikanaji wa maji, hususan katika maeneo ya vijijini, na kwamba utekelezaji wa Mradi wa Miji 28 ndiyo suluhisho muhimu litakalosaidia kumaliza tatizo hilo kwa kiasi kikubwa.


Kasaka ameyasema hayo Julai 18, 2026, alipokuwa akizungumza na waandishi wa habari kuhusu hali ya upatikanaji wa maji katika Wilaya ya Chunya, hasa maeneo ya vijijini ambayo bado yanakabiliwa na uhaba wa huduma hiyo muhimu.


Amesema kukamilika kwa Mradi wa Miji 28 kutaiwezesha Serikali kuanza kusambaza maji katika vijiji mbalimbali na baadaye kufikisha huduma hiyo hadi kwenye vitongoji, hatua ambayo itasaidia kuhakikisha wananchi wengi zaidi wanapata maji safi na salama.


 “Mradi huu utakapokamilika tutaanza kusambaza maji kwenye vijiji na baadaye kwenye vitongoji ili wananchi wote waweze kupata huduma ya maji safi na salama,” amesema Kasaka.


Mbunge huyo amesema Serikali tayari imetenga Dola milioni tano kwa ajili ya uchimbaji wa visima katika maeneo yanayolengwa, huku taratibu zikiendelea za kutafuta fedha zaidi kwa ajili ya kukamilisha utekelezaji wa mradi huo.


Kwa upande wake, Diwani wa Kata ya Chokaa, Joshua Mwambalala, amesema kutokana na umuhimu wa maji katika maisha ya wananchi, wataendelea kushirikiana na Serikali kuhakikisha changamoto hiyo ya muda mrefu inapatiwa ufumbuzi.


Mwambalala amesema kabla ya kuwa diwani alikuwa Mwenyekiti wa Kitongoji kwa kipindi cha miaka kadhaa, hivyo anafahamu kwa kina changamoto zinazowakabili wananchi, hususan katika upatikanaji wa maji.


 “Kabla ya kuwa diwani nilihudumu kama Mwenyekiti wa Kitongoji kwa miaka kadhaa, hivyo ninazifahamu changamoto nyingi za wananchi. Nina imani na Mbunge wetu pamoja na Serikali iliyopo madarakani katika kutatua kero hii ya maji,” amesema.


Mwisho.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3