Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MAKONDA AIPONGEZA CRDB, AZINDUA MSIMU WA NNE WA ZOGO MCHONGO

MAKONDA AIPONGEZA CRDB, AZINDUA MSIMU WA NNE WA ZOGO MCHONGO

 


Na Matukio DaimaMedia 


Dar es Salaam. Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, Paul Makonda, ameipongeza Benki ya CRDB kwa kutumia ubunifu kuwafikishia Watanzania elimu ya fedha kupitia kipindi cha Zogo Mchongo, akisema hatua hiyo inachangia kuongeza uelewa wa kifedha na kuunga mkono juhudi za Serikali za kujenga uchumi shirikishi.


Akizungumza jijini Dar es Salaam wakati wa uzinduzi wa msimu wa nne wa kipindi hicho, Makonda alisema elimu ya fedha imeendelea kuwa nyenzo muhimu katika kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu uwekezaji, biashara, matumizi na utunzaji wa fedha.


Alisema Serikali kupitia Benki Kuu ya Tanzania (BoT) imeendelea kuhimiza utoaji wa elimu ya fedha kwa wananchi, huku CRDB ikiwa miongoni mwa taasisi za kifedha zilizofanikiwa kuifikisha elimu hiyo kwa njia bunifu kupitia televisheni, mitandao ya kijamii na ushirikiano na wasanii, wanamichezo pamoja na watengeneza maudhui.


Makonda alisema matumizi ya watu wenye ushawishi katika jamii yameongeza ufanisi wa kufikisha ujumbe wa elimu ya fedha kwa makundi mbalimbali, hususan vijana, huku yakifungua fursa za ajira na kuongeza kipato kupitia sekta ya ubunifu.



Aidha, aliwahimiza Watanzania kutumia muda wao kujifunza masuala ya fedha, biashara na uwekezaji badala ya kufuatilia taarifa zisizo na manufaa, akieleza kuwa hatua hiyo itawawezesha kunufaika zaidi na fursa mbalimbali za kiuchumi zinazojitokeza nchini.


Pia alisema matukio makubwa yanayotarajiwa kufanyika nchini yanapaswa kutazamwa kama fursa za kuongeza kipato, akisisitiza kuwa wananchi watanufaika zaidi iwapo watakuwa na uelewa mzuri wa masuala ya fedha na namna ya kuzitumia fursa hizo.



Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Benki ya CRDB, Abdulmajid Nsekela, alisema benki hiyo imepanua mkakati wake kutoka kutoa huduma za kifedha pekee hadi kujenga jamii yenye maarifa ya fedha, ili kuwawezesha wananchi kufanya maamuzi sahihi kuhusu huduma za kifedha.


Alisema kipindi cha Zogo Mchongo ni sehemu ya mkakati huo, ambapo kupitia msimu wa nne wananchi wataendelea kupata elimu kuhusu uwekezaji, usimamizi wa fedha binafsi na matumizi sahihi ya huduma za kifedha, kwa lengo la kukuza ustawi wa mtu mmoja mmoja na maendeleo ya uchumi wa taifa.




Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3