LISSU NA MCH MSIGWA WAKUTANA MAHAKAMANI KWA MARA YA KWANZA BAADA YA MSIGWA KURUDI CHADEMA.
Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (Chadema), Tundu Lissu, ameendelea kujitetea katika kesi ya kikatiba iliyofunguliwa dhidi ya Mamlaka ya Magereza, huku Mahakama ikisikiliza ushahidi wa shahidi wa nne na wa mwisho wa upande wa wajibu maombi.
Shahidi huyo ni Mkuu wa Gereza la Ukonga, ambaye amefika mahakamani kutoa ushahidi kuhusu madai yaliyowasilishwa katika kesi hiyo.
Kesi hiyo ilifunguliwa na mawakili Nashon Nkungu, Paul Kisabo na Kulwa Maduhu, wakipinga vikwazo wanavyodai wamekuwa wakikumbana navyo wanapomtembelea Lissu gerezani na kufanya mashauriano ya kisheria.
Usikilizwaji wa kesi hiyo umeendelea kwa siku nne mfululizo. Katika siku zilizopita, Lissu alimaliza kumuhoji shahidi wa tatu kabla ya Mahakama kuendelea na ushahidi wa Mkuu wa Gereza la Ukonga.
Aidha Tundu Lissu, amekutana na aliyekuwa mbunge wa Iringa Mjini, Peter Msigwa, katika Mahakama Kuu ya Tanzania jijini Dar es Salaam, ikiwa ni mara ya kwanza wawili hao kuonekana pamoja hadharani tangu Msigwa arejee Chadema.
Wawili hao walionekana wakikumbatiana muda mfupi baada ya mahakama kuahirisha kwa muda usikilizwaji wa shauri lililowasilishwa na mawakili wawili wanaojitambulisha kuwa washauri wa kisheria wa Lissu.
Msigwa, ambaye aliwahi kuwa mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Nyasa, alifika mahakamani kufuatilia mwenendo wa shauri hilo.
Katika kesi hiyo, mawakili hao wanapinga kile wanachodai kuwa ni vikwazo vinavyowazuia kufanya mazungumzo ya siri ya kisheria na mteja wao, Tundu Lissu, ambaye anashikiliwa katika Gereza la Ukonga.
Msigwa alihama Chadema na kujiunga na Chama Cha Mapinduzi, CCM, mwezi Juni mwaka 2024 kabla ya kurejea tena Chadema tarehe 23 Mei 2026.
Kuonekana kwake katika Mahakama Kuu kunatajwa kuwa tukio la kwanza la hadhara akiwa pamoja na Lissu tangu alipojiunga tena na chama hicho cha upinzani.
Wakati huo huo, Mwenyekiti wa Chadema Kanda ya Pwani, Boniface Jacob maarufu kama Boni Yai, amemfananisha mwanasiasa Peter Msigwa na kiungo wa Simba SC, Clatous Chama, kufuatia uamuzi wa Msigwa kurejea Chadema baada ya kuondoka CCM.
Akizungumza mbele ya wanachama na wafuasi wa chama hicho, Boni Yai alisema kurejea kwa Msigwa kunafanana na jinsi Clatous Chama alivyorejea Simba SC baada ya kipindi cha kuichezea klabu nyingine.
''Sasa subirini magoli 50'', anasema Boniface Jacob.
Shauri hilo, linalohusu haki ya mawakili kupata fursa ya kufanya mawasiliano ya siri na mteja wao (Lissu), limeahirishwa kwa muda, huku mahakama ikitarajiwa kutoa mwelekeo wa hatua zinazofuata.
Haya yanajiri baada ya wito kutoka Jumuiya ya Madola ikitaka Lissu aachiliwe huru ndani ya siku 28.