KAPOMA: SERIKALI IWEKE MAZINGIRA MAZURI KWA WATAALAMU WA AFYA
Jul 25, 2026
Na Matukio Daima Media, Morogoro.
Mbunge wa Viti Maalum Mkoa wa Morogoro, Josephine Kapoma, ameishauri Serikali kuweka mazingira salama na mazuri kwa wataalamu wa afya wanaohitimu ili waweze kutumia taaluma zao kutoa huduma kwa wananchi, hususan katika maeneo ya vijijini na pembezoni.
Kapoma amesema Serikali imefanya mambo makubwa sana katika sekta ya afya kwa kujenga hospitali, vituo vya afya na zahanati, lakini bado mafanikio hayo hayatakuwa na maana kama wataalamu wengi watakuwa hawapendi kwenda kufanya kazi vijijini kutokana na changamoto ya miundombinu, hasa kukosekana kwa makazi mazuri ya watumishi.
Amesema Serikali imewekeza zaidi katika ujenzi wa vituo vya kutolea huduma za afya, lakini suala la makazi ya watumishi limeonekana kusahaulika, jambo linaloweza kuwafanya wataalamu kusita kwenda kufanya kazi katika maeneo hayo.
Kapoma ameitaka Serikali kuliangalia suala la makazi kwa jicho la kipekee, hasa katika maeneo ya pembezoni, ili kuhakikisha wataalamu wanapatikana na wananchi wanapata huduma bora za afya karibu na maeneo yao.
Akizungumzia programu mpya ya Tiba Lishe, Kapoma amesema kuanzishwa kwake ni hatua muhimu kuelekea Dira ya Maendeleo ya Taifa ya 2050, kwa kuwa inalenga kukabiliana na changamoto ya magonjwa yanayotokana na lishe duni.
Amesema Serikali inapaswa kuhakikisha wahitimu wa programu hiyo na fani nyingine za afya wanapata mazingira mazuri na salama ya kufanya kazi ili waweze kutumia elimu waliyoipata kwa manufaa ya wananchi.
Mkuu wa Chuo cha Afya na Sayansi Shirikishi Morogoro, Evarist Urasa, amesema programu ya Tiba Lishe imeanzishwa kwa lengo la kuandaa wataalamu watakaosaidia jamii kukabiliana na ongezeko la magonjwa yasiyo ya kuambukiza.
Urasa amesema kabla ya kuanzishwa kwa programu hiyo, Wizara ilifanya utafiti na kubaini uhitaji wa wataalamu hao, huku vyuo viwili nchini vikiruhusiwa kuanza kutoa mafunzo hayo.
Amesema wahitimu wataandaliwa kufanya kazi katika ngazi za zahanati, vituo vya afya na hospitali, pamoja na kujiajiri kwa kutoa elimu na huduma za Tiba Lishe.
Naye mhitimu wa fani ya Maabara, Clara Kihongole, amewataka vijana kutosubiri ajira za Serikali pekee, bali kutumia elimu na ujuzi waliopata vyuoni kujiajiri na kutumia taaluma zao kutatua changamoto zilizopo katika jamii.
Mwisho



