Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
JUMUIYA YA MADOLA YAIPA SERIKALI YA TANZANIA SIKU 30 KUMWACHIA HURU TUNDU LISSU

JUMUIYA YA MADOLA YAIPA SERIKALI YA TANZANIA SIKU 30 KUMWACHIA HURU TUNDU LISSU

 


Serikali ya Tanzania imepewa siku 30 na Kikundi cha Mawaziri cha Jumuiya ya Madola (CMAG) kutatua suala la kuzuiliwa kwa Mwenyekiti wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) taifa, Tundu Lissu kupitia njia za kisiasa na kisheria, na kuwaachia huru watu wengine wanaoshikiliwa kwa sababu ya kutumia kile kilichotajwa na Jumuiya hiyo kama haki zao kwa amani.


Maelekezo hayo yametolewa Julai 10, 2026 katika mkutano wa pamoja wa dharura wa CMAG ulioambatana na kutolewa tamko hilo ambalo limetaka pia kufanyika kwa jukwaa la mashauriano linaloshirikisha vyama vyote vya siasa Tanzania ndani ya siku 90 ili kujadili mageuzi ya mfumo wa uchaguzi, ushindani wa kisiasa, masuala ya mahabusu na uwajibikaji, na ndani ya siku 60 irejeshe uhuru kamili wa matumizi ya mitandao ya kijamii.


CMAG pia imeamua kuendelea kuiweka Tanzania kwenye ajenda yake rasmi, ikisema pamoja na hatua chache zilizopigwa tangu maamuzi ya mkutano wake wa Desemba 5, 2025, bado yapo maeneo muhimu ambayo hayajatekelezwa. Kikundi hicho kimetaka kuondolewa kwa vikwazo vinavyohusu uhuru wa kukusanyika, kujieleza, shughuli za asasi za kiraia na vyombo vya habari, kufanyika kwa mazungumzo ya kisiasa kati ya vyama, pamoja na kuwepo kwa uwajibikaji kwa wahusika wa matukio ya vurugu na fidia kwa waathirika pale inapostahili.


Hata hivyo, Serikali ya Tanzania kupitia kauli za viongozi wake wa ngazi ya juu imekuwa ikisisitiza mara kadhaa kuwa haiwezi kuingilia mwenendo wa shauri la Tundu Lissu kwa kuwa suala hilo liko mahakamani, wamekuwa wakieleza kuwa Tanzania ni nchi huru na yenye mamlaka kamili ya kujiamulia mambo yake ya ndani hasa utawala wa nchi, utekelezaji wa sheria na masuala ya ndani ambayo yanaendeshwa kwa mujibu wa Katiba na sheria za Tanzania, bila kushinikizwa au kuamuliwa na mataifa au taasisi za nje.


Tamko hili limejiri baada ya mkutano huo kupokea ripoti ya Katibu Mkuu wa Jumuiya ya Madola kuhusu ziara ya Mjumbe wake Maalum nchini Tanzania, Dkt. Lazarus McCarthy Chakwera (Rais mstaafu wa Malawi) ya mwezi Aprili, 2026. Wakati wa ziara hiyo, Chakwera alikutana na Rais Samia Suluhu Hassan, viongozi wa Serikali, viongozi wa vyama vya siasa, wawakilishi wa asasi za kiraia, viongozi wa dini, Tume ya Uchunguzi ya Matukio ya Wakati na Baada ya Uchaguzi wa Oktoba 29 pamoja na wadau wengine.


CMAG imekubali kukutana tena kwa dharura mwezi Septemba 2026 kupokea ripoti ya maendeleo kutoka Tanzania. Katika mkutano wa Novemba 2026, CMAG itafikiria kuchukua hatua zaidi iwapo hakutakuwa na maendeleo yaliyotarajiwa.


Aidha CMAG imesema Jumuiya ya Madola iko tayari kutoa msaada wa kiufundi kwa maombi ya Tanzania na itandelea kushirikiana na Umoja wa Afrika (AU), SADC, EAC, na Umoja wa Mataifa (UN).



Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3