Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
 ELIMU YA USAFI WA PAMBA YAONDOA IMANI POTOFU, KUONGEZA UZITO WA PAMBA KWA MAJI NA MAFUTA YA KENGE.

ELIMU YA USAFI WA PAMBA YAONDOA IMANI POTOFU, KUONGEZA UZITO WA PAMBA KWA MAJI NA MAFUTA YA KENGE.


NA CHAUSIKU SAID 

MATUKIO DAIMA.

Kwa miaka mingi, baadhi ya wakulima wa zao la pamba wilayani Bariadi Mkoani Simiyu walikuwa wakiamini kuwa kuongeza maji, mchanga na mafuta ya kenge kwenye pamba kuliongeza uzito wa zao hilo na hivyo kuwaongezea kipato.

Imani hiyo ilichochewa na matumizi ya mizani ya zamani iliyokuwa ikilalamikiwa kwa kutokuwa sahihi, hali iliyowafanya baadhi ya wakulima kutafuta mbinu za kujiongezea uzito wa pamba kabla ya kuipeleka sokoni.

Lakini leo, simulizi hiyo inaanza kubaki historia, Kupitia elimu inayotolewa na Bodi ya Pamba kwa kushirikiana na AMCOS, viongozi wa vijiji na vijana wa BBT, wakulima wameanza kuelewa kuwa si maji, mchanga wala mafuta ya kenge yanayoongeza thamani ya pamba, bali usafi na ubora wa zao hilo tangu linapovunwa shambani hadi linapofika sokoni.

Mabadiliko hayo yanashuhudiwa na mkulima wa kijiji cha Isuyu, kata ya Igirya wilayani Bariadi, Philipo Isucha, ambaye anasema mafunzo hayo yamebadili namna wanavyolima, kuvuna na kuhifadhi pamba.

"Ili kupata pamba safi inabidi kupalilia kwa wakati, kupulizia dawa kwa wakati ili kuua wadudu wanaoharibu pamba na kuifanya iwe kwenye ubora wa gredi A ,tumepata elimu ya kulima pamba na kuiboresha ili ikubalike sokoni,

 Pamba ikishachanua tunatakiwa kuivuna mapema, na tunapoenda kuuza isiwekewe maji, mchanga wala mafuta ya kenge kwa sababu vitu hivyo vinaharibu ubora wa pamba."Amasema Isucha.

Mbali na kubadili namna ya uzalishaji, elimu hiyo imewasaidia wakulima kuelewa kuwa uchafuzi wa pamba hauongezi uzito wa kweli, bali husababisha kushuka kwa ubora wake na wakati mwingine pamba hukataliwa au mkulima hukatwa fedha anapoipeleka sokoni.

Hilo linathibitishwa na mkulima Sumbuko Dahinda wa kijiji cha Isuyu, anayesema zamani ilikuwa kawaida kuona wakulima wakitumia maji mchanga au mafuta ya kenge kabla ya kuuza pamba, lakini hali hiyo imebadilika.

"Serikali imepambana kulirudisha zao hili kwa kutuletea dawa na elimu ya utunzaji wa pamba, Zamani mtu alikuwa akitaka kwenda kuuza pamba lazima alowanishe shuka la kufungia pamba kwa maji au mafuta ya kenge, lakini baada ya elimu watu wanavuna pamba nzuri na ili pamba ipande bei lazima uvunaji uwe mzuri."Amesema Dahinda.

Ili kuhakikisha mabadiliko hayo yanaendelea kudumu, AMCOS zimepewa jukumu la kuwafundisha wakulima namna sahihi ya kuhifadhi pamba baada ya kuvuna, kwa kuondoa tabia zilizokuwa zikiharibu ubora wa zao hilo.

Mwenyekiti wa AMCOS Isuyu, Mwalu Nindwa, anasema elimu hiyo imewafanya wakulima kuacha kuhifadhi pamba sehemu chafu na kuitunza katika mazingira yanayolinda ubora wake.

"Tulipewa elimu ya namna ya kusimamia zao la pamba na kuwafundisha wakulima kuhifadhi pamba sehemu safi. Zamani watu walikuwa wanaifanya pamba kitanda cha watoto na watoto walikuwa wanaikojolea humo humo. Sasa wakulima wanaelewa kuwa pamba ikihifadhiwa sehemu safi ndiyo inapata gredi A."Amesema Nindwa.

Kwa upande wake, Diana Daud wa BBT anasema wameendelea kufikisha elimu hiyo moja kwa moja mashambani ili kuhakikisha kila mkulima anaelewa hatua za kufuata kuanzia uvunaji hadi uhifadhi wa pamba.

 "Tumekuwa tukiitisha vikao na kutoa elimu kwa wakulima kuhusu namna bora ya kuvuna pamba. Anapoona pamba imepasuka ahakikishe anaivuna kwa kutumia kifaa kisafi na anapoifikisha nyumbani aiweke sehemu safi mpaka atakapoipeleka sokoni."Amesema Diana.

Akizungumzia matokeo ya kampeni hiyo ya elimu, Mkaguzi wa Pamba kutoka Bodi ya Pamba wilaya ya Bariadi Mkoani Simiyu, Ndinda Antony, anasema katika msimu huu wamewafikia wakulima kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji, AMCOS na vijana wa BBT ili kuhakikisha kila mkulima anaelewa umuhimu wa kuzalisha pamba safi inayokidhi viwango vya ubora vinavyohitajika ndani na nje ya nchi.

"Tulipita kwa wakulima tukawapa elimu kwa kushirikiana na viongozi wa vijiji, wakulima wawezeshaji, BBT pamoja na AMCOS zote 74 zilizopo wilayani Bariadi. Lengo letu lilikuwa kuhakikisha mkulima anazalisha pamba inayokidhi usafi na ubora unaohitajika sokoni, na kwa kiasi kikubwa wakulima wameendelea kuzingatia elimu hiyo."Amesema Anthony.

Antony amesema matokeo ya elimu hiyo tayari yanaonekana, ambapo tathmini ya kitaifa ya msimu wa ununuzi wa pamba wa mwaka 2025/2026 imeonyesha ubora wa pamba umeongezeka kutoka asilimia saba hadi asilimia 21, huku lengo la msimu huu likiwa ni kufikia zaidi ya asilimia 75 ili pamba ya Tanzania iweze kupata thamani kubwa katika soko la dunia.

"Tukifikia zaidi ya asilimia 75 ya usafi na ubora wa pamba, marobota yetu yatapata gredi A na thamani inayotakiwa katika soko la kimataifa hii itasaidia kuongeza ushindani wa pamba ya Tanzania na hatimaye mkulima kupata manufaa ya jasho lake."Amesema Anthony.

Hata hivyo, anaeleza kuwa bado kuna baadhi ya wakulima wanaoamini kuwa kuweka maji, mchanga na mafuta ya kenge kunaongeza uzito wa pamba, jambo ambalo si la kweli kwani uzito wa pamba hutokana na kuzingatia kanuni bora za kilimo, ikiwemo kuvuna kwa wakati na kuiacha pamba ibaki katika uzito wake wa asili.


"Tunawaambia wakulima waachane na dhana ya kuchafua pamba kwa lengo la kuongeza kilo. Pamba ina uzito wake wa asili, na kilo zinaongezeka kwa kuzingatia kanuni bora za kilimo, kuvuna kwa wakati na kuhifadhi pamba katika mazingira safi. Tukichafua pamba ya Bariadi, tunakuwa tumeharibu sifa ya pamba ya Tanzania nzima."Alisema Anthony.

Antony anaeleza kuwa serikali itaendelea kuwekeza katika sekta ya pamba kwa kusambaza pembejeo kwa wakati, kuimarisha huduma za ugani, kutumia teknolojia za kudhibiti wadudu na kuanzisha kiwanda cha mbolea hai, hatua ambazo zinatarajiwa kuongeza uzalishaji kutoka kilo milioni 18.2 zilizozalishwa msimu uliopita hadi kufikia kilo milioni 20 katika msimu ujao.

mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3