Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
BODI YA KOROSHO WAPIGIA DEBE ELIMU YA KUPAMBANA NA MAGONJWA, WADUDU.

BODI YA KOROSHO WAPIGIA DEBE ELIMU YA KUPAMBANA NA MAGONJWA, WADUDU.

Matukio Daima, Morogoro 

WAKATI Tanzania ikiendelea kuongeza juhudi za kukuza uzalishaji wa korosho, Bodi ya Korosho Tanzania kupitia  wataalamu mbalimbali wa kilimo wamesisitiza kuwa ushindi dhidi ya wadudu na magonjwa ya zao hilo utawezekana ikiwa wakulima watapata elimu sahihi ya kilimo bora kupitia maafisa ugani waliopo karibu nao.

Morogoro ni miongoni mwa mikoa inayoendelea kuimarisha uwezo wa maafisa kilimo kupitia mafunzo maalumu yanayotolewa na Bodi ya Korosho, yanayolenga kuwajengea uelewa wa mbinu bora za kudhibiti wadudu na magonjwa ya korosho, hatua inayotarajiwa kuongeza uzalishaji, ubora wa zao hilo na kipato cha wakulima.

Akizungumza wakati wa mafunzo yaliyotolewa maeneo mbalimbali ya wilaya za Mvomero na Ulanga, Mkufunzi wa Chuo cha Mafunzo ya Kilimo Mtwara, Joseph Mkude, anasema kutofuata kanuni za kilimo bora kunachangia upotevu mkubwa wa mavuno, hivyo maafisa kilimo wanapaswa kuhakikisha elimu hiyo inawafikia wakulima katika kila kijiji.

Naye Mtafiti kutoka Taasisi ya Utafiti wa Kilimo Tanzania, TARI, Naliendele, George Lucas, amesema matumizi ya mbegu bora, ufuatiliaji wa mashamba na tafiti zinazoendelea kufanyika vitasaidia kuongeza uwezo wa wakulima kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi pamoja na wadudu waharibifu.


Afisa Kilimo wa Bodi ya Korosho Tanzania, Tawi la Morogoro, Edson Mbande, akizungumza na maafisa Kilimo wa Mvomero kwenye elimu va vitendo mashambani juu ya upuliziaji dawa na kubaini viashiria vya wadudu na magonjwa kwenye mikorosho, anasema ushirikiano kati ya taasisi mbalimbali unalenga kuhakikisha wakulima wanazalisha korosho nyingi zenye ubora unaokidhi mahitaji ya soko.





Kwa upande wake, Afisa Kilimo wa Mamlaka ya Afya ya Mimea na Viuatilifu Tanzania,TPHPA, Kaizer Kaluwa, anasisitiza matumizi ya viuatilifu vinavyokubalika na maandalizi bora ya mashamba, huku Afisa Kilimo wa Kata ya Mlali, Amanda Hilary, akisema elimu hiyo sasa wataipeleka ngazi ya kata na vijiji ili kuwafikia wakulima wengi zaidi.

Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3