ACT WAZALENDO YAIBANA SERIKALI KUKAMATWA KWA WAHADHIRI WA VYUO VIKUU
Na Matukio DaimaMedia
ACT Wazalendo imeibana Serikali kuhusu kukamatwa kwa baadhi ya wahadhiri wa vyuo vikuu nchini, ikisema hatua hizo zinadhoofisha uhuru wa taaluma na kuhatarisha ubora wa elimu ya juu nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dar es Salaam, Waziri Kivuli wa Elimu, Sayansi na Teknolojia wa ACT Wazalendo, Riziki Shari Mngwali, alisema Tanzania imeridhia mikataba mbalimbali ya kimataifa, kikanda na ya Afrika inayolinda uhuru wa taaluma, hivyo Serikali ina wajibu wa kuhakikisha wanataaluma wanatekeleza majukumu yao katika mazingira salama na yenye uhuru wa kujieleza.
Mngwali amesema chama hicho kinalaani kukamatwa kwa wahadhiri akiwemo Melkzedeki Kaijage wa Chuo Kikuu cha Dodoma (UDOM), pamoja na Johaiven Revelian Bikongolo na Titus Joseph Kituli wa Chuo Kikuu cha St. John University of Tanzania (SJUT), akisisitiza kuwa masuala ya kitaaluma na kinidhamu yanapaswa kushughulikiwa kupitia taratibu na mamlaka za vyuo husika.
Amesema kuwa, kuendelea kwa matukio hayo kunazua hofu kwa wahadhiri na wanafunzi, jambo ambalo linaweza kudhoofisha mijadala ya kitaaluma na kuathiri uwezo wa vyuo vikuu kuzalisha maarifa, tafiti na suluhisho kwa changamoto za maendeleo ya taifa.
"Vyuo vikuu ni kitovu cha fikra na tafiti, wanataaluma wanapaswa kuwa huru kufundisha, kufanya utafiti na kujadili masuala ya kitaaluma bila hofu, mradi wanazingatia sheria na maadili ya taaluma," amesema Mngwali.
Kutokana na hali hiyo, ACT Wazalendo imeitaka Serikali kuheshimu uhuru wa taaluma, kulinda mamlaka ya vyuo vikuu na kuhakikisha taasisi za elimu ya juu zinaendelea kuwa mazingira salama ya kufundisha, kujifunza na kufanya tafiti kwa manufaa ya taifa.
