Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WASHIRIKI 100 WAFUZU VIJANA CHALLENGE 2026

WASHIRIKI 100 WAFUZU VIJANA CHALLENGE 2026

 

Na Hamida Ramadhan, matukio daima Media Dodoma

WASHIRIKI 100 wamefanikiwa kuingia hatua ya pili ya shindano la Vijana Uchumi Challenge 2026 baada ya kupitia mchujo mkali ulioshirikisha maelfu ya vijana kutoka maeneo mbalimbali nchini.

Akizungumza wakati wa kutangaza matokeo hayo, Katibu wa Kamati ya Kitaifa ya shindano hilo, Amina Sanga, alisema jumla ya maombi 7,852 yalipokelewa, yakionesha mwamko mkubwa wa vijana kushiriki katika kutafuta suluhisho na fursa za kukuza uchumi wa Taifa.

Ameeleza kuwa shindano hilo lina lengo la kuhamasisha ubunifu miongoni mwa vijana na kuibua mawazo yenye uwezo wa kuchochea maendeleo ya kiuchumi, sambamba na kuunga mkono juhudi za Serikali katika kufanikisha Dira ya Taifa ya Maendeleo 2050.

Kwa mujibu wa takwimu zilizotolewa, mawazo mengi yaliyowasilishwa yalitoka katika sekta ya teknolojia na huduma za kidigitali, ikifuatiwa na kilimo pamoja na ubunifu wa teknolojia za kilimo, huku sekta ya uzalishaji na viwanda nayo ikitoa mchango mkubwa.

Sanga amesema zaidi ya nusu ya maombi yote yaliyowasilishwa yalitimiza vigezo vya msingi vya ushiriki, na baada ya hatua mbalimbali za tathmini, washiriki 100 ndio waliopata nafasi ya kuendelea mbele kutokana na ubora na uwezo wa mawazo yao kuleta matokeo chanya katika uchumi wa nchi.

Washiriki hao wanatarajiwa kushiriki mafunzo maalum yatakayowajengea uwezo wa kuendeleza na kuwasilisha mawazo yao kwa ufanisi zaidi

" Baada ya mafunzo hayo, wataendelea kuchujwa hadi kupatikana washiriki 30 wa hatua ya nusu fainali na baadaye 10 watakaowania ushindi wa mwisho, " Amesema.

Waandaaji wa shindano hilo pia wametangaza ongezeko la zawadi, ambapo mshindi wa kwanza atajinyakulia Sh milioni 50, mshindi wa pili Sh milioni 30 na mshindi wa tatu Sh milioni 20. 

Mbali na zawadi hizo, washiriki wote 100 waliofuzu watapata vyeti vya utambuzi, mafunzo ya kitaalamu na fursa za kuunganishwa na wadau mbalimbali kwa ajili ya kukuza mawazo yao

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3