VIKUNDI 101 VYAPOKEA MKOPO WA ZAIDI YA BILIONI 1.2 KUTOKA JIJI LA ARUSHA.
Na,Jusline Marco:Arusha
Zaidi ya Shilingi bilioni 1.2 zimetolewa kwa vikundi 101 vya vijana, wanawake na watu wenye ulemavu kupitia mpango wa mikopo ya asilimia 10 ya mapato ya ndani kwa robo ya tatu ya mwaka wa fedha 2025/2026.
Akikabidhi hundi za mikopo hiyo kwa wanufaika, Mkuu wa Wilaya ya Arusha, Joseph Mkude amesema Mikopo hiyo inalenga kuwezesha makundi hayo kuanzisha, kuendeleza na kupanua shughuli za kiuchumi zitakazoongeza kipato na kuboresha maisha yao.
Aidha amevipongeza vikundi hivyo kwa kufanikiwa kufikia hatua ya kupata mikopo hiyo,huku akieleza kuwa fursa hiyo imepatikana baada ya kutimiza masharti na taratibu zilizowekwa ambapo amebainisha kuwa baadhi ya waombaji hukosa nafasi kutokana na kukosa nidhamu, uvumilivu na ufuatiliaji wa mahitaji muhimu ya mpango huo.
Mkude amewataka wanufaika hao kutumia fedha hizo kwa malengo yaliyokusudiwa ili ziweze kuleta matokeo chanya katika biashara na miradi yao ya uzalishaji mali,na kuwahimiza kurejesha mikopo hiyo kwa wakati ili kuifanya programu hiyo kuwa endelevu na kuwezesha vikundi vingine kunufaika katika awamu zijazo.
Utoaji wa mikopo hiyo ni sehemu ya juhudi za Serikali chini ya uongozi wa Rais wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, za kuhakikisha wananchi wanapata mitaji na fursa za kiuchumi zinazowawezesha kujitegemea na kuinua hali zao za maisha ambapo Serikali pia imeendelea kusimamia utekelezaji wa mpango wa mikopo ya asilimia 10 kwa lengo la kuwajengea uwezo wananchi na kuchochea maendeleo ya uchumi katika ngazi za jamii.


