WANU AMPONGEZA MBUNGE UKONGA KWA KUFADHILI VIJANA ZAIDI YA 200 KUPATA ELIMU
Na Matukio Daima Media
Naibu waziri wa elimu,sayansi na teknolojia Wanu Hafidh Ameir ameipongeza jitihada zinazofanywa na Mbunge wa Ukonga,Bakari Shingo katika kuinua elimu kwa vijana wa Jimbo la Ukonga kwa kuwafadhili ili kupata elimu ya ufundi ili kujikwamua kiuchumi.
Akizungumza katika Mahafali ya 18 ya Chuo cha Ufundi na Mafunzo ya Ufundi Stadi Furahika kilichopo Buguruni Malapa, Ilala jijini Dar es Salaam, Naibu Waziri huyo wa amesema kuwa ufadhili wa mbunge huyo kwa vijana hao ni matokeo ya ushirikiano thabiti kati yake na serikali.
"niikipongeze chuo hiki kwa juhudi mnazofanya kutoa ujuzi kwa vijana wetu, lakini pia Mbunge wa Jimbo la Ukonga Mhe. Bakari Shingo nimeambiwa hapa unasomesha wanafunzi 220 ambao wengine wamehitimu leo, haya ni mafanikio makubwa yanayotokana na ushirikiano mzuri ulipo baina yenu na Serikali," ameongeza Naibu Waziri Wanu.
Aidha amesmema serikali itaendelea kuimarisha elimu ya ujuzi na umahiri ili kuwajengea vijana uwezo wa kujiajiri na kuhimili ushindani wa soko la ajira, huku ikilenga kuwafikia vijana 80,000 kupitia Programu ya Mama Samia ya Utambuzi na Urasimishaji wa Ujuzi ifikapo Juni 2027.
amesema vijana wanapaswa kuchangamkia program hiyo kwa kuwa inalenga kutambua, kuthibitisha na kurasimisha ujuzi walioupata kupitia uzoefu wa kazi, mafunzo kazini na njia nyingine zisizo rasmi za kujifunza.
Kwa upande wake Mbunge wa Jimbo la Ukonga , Bakari Shingo amesema mpaka sasa ameshafadhili wanafunzi 220 katika Chuo hicho akitumia utaratibu wa kutangaza fursa hizo kupitia gari la matangazo ili kutoa nafasi kwa kila kijana anayehitaji kupata ujuzi.
Amesema ataendelea kuhakikisha katika kipindi cha uongozi wake kama mwakilishi wa wananchi anatoa fursa kwa makundi mbalimbali katika Jimbo lake kwa kuwawezesha katika nyanja mbalimbali.





