TAKUKURU MOROGORO YABAINI DOSARI, YAKUSANYA MILIONI 69
Na Lilian Kasenene, Morogoro
Matukio DaimaApp
NAIBU Mkuu wa Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU) Mkoa wa Morogoro, Christopher Mwakajinga amesema taasisi hiyo imefanikiwa kusaidia kukusanya zaidi ya Shilingi milioni 69 ambazo hazikuwa zimekusanywa kutokana na dosari zilizobainika katika mfumo wa ukusanyaji wa mapato.
Mwakajinga ameyasema hayo wakati akiwasilisha taarifa ya utendaji ya TAKUKURU Mkoa wa Morogoro kwa kipindi cha Januari hadi Machi, 2026 kwa vyombo vya habari, ambapo alisema kiasi cha Shilingi 69,248,392 kilikusanywa baada ya taasisi hiyo kufanya operesheni maalumu ya ufuatiliaji wa makusanyo ya mapato kupitia mashine za POS zinazotumia mfumo wa TAUSI.
Alisema uchunguzi uliofanywa ulibaini kuwepo kwa kutokuwiana kwa taarifa za makusanyo kati ya mfumo wa TAUSI na taasisi za kifedha, hali iliyosababisha kuonekana kwa madeni yasiyo halisi katika rekodi za wakusanyaji wa mapato. Kufuatia mapendekezo yaliyotolewa na TAKUKURU, changamoto hizo zilirekebishwa na fedha husika kukusanywa.
Katika hatua nyingine, Mwakajinga alisema TAKUKURU Morogoro ilifuatilia utekelezaji wa miradi minane ya maendeleo yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 2.7 kwa lengo la kuhakikisha fedha za umma zinatumika kwa ufanisi na kuzingatia thamani halisi ya fedha.
Alisema kupitia ushauri wa kitaalamu uliotolewa na taasisi hiyo, matumizi yenye thamani ya zaidi ya Shilingi bilioni 15.7 yaliokolewa au kurejeshwa katika miradi mbalimbali ya maendeleo, hususan katika sekta za elimu, afya na maji.
Akizungumzia elimu kwa umma, Mwakajinga alisema TAKUKURU imeendelea kuhamasisha wananchi kushiriki katika mapambano dhidi ya rushwa kupitia semina, mikutano ya hadhara na vyombo vya habari. Katika kipindi hicho, taasisi hiyo ilifanya semina 74, mikutano ya hadhara 19, ilihamasisha uanzishwaji na uimarishaji wa klabu 100 za kupinga rushwa, pamoja na kutoa taarifa mbili kwa vyombo vya habari na kushiriki vipindi viwili vya redio.
Aidha, alisema TAKUKURU ilipokea jumla ya malalamiko 94 kutoka kwa wananchi, ambapo kati ya hayo malalamiko 65 yalihusu tuhuma za vitendo vya rushwa na kuanza kufanyiwa kazi. Malalamiko mengine 29 yalihusu masuala yasiyo ya rushwa na yalielekezwa kwenye mamlaka husika kwa hatua zaidi.
Mwakajinga aliwataka wananchi kuendelea kushirikiana na TAKUKURU kwa kutoa taarifa za vitendo vya rushwa vinavyofanyika katika maeneo yao ili kusaidia juhudi za serikali katika kuimarisha uwajibikaji, uwazi na utawala bora.
Alisema wananchi wanaweza kutoa taarifa za rushwa kupitia namba ya bure 113, simu 0738 150 143 au kufika katika ofisi za TAKUKURU zilizopo karibu nao.
Alisisitiza kuwa mapambano dhidi ya rushwa yanahitaji ushiriki wa kila mwananchi, akirejea kauli mbiu ya taasisi hiyo inayosema, “Kuzuia Rushwa ni Jukumu lako na langu, tutimize wajibu wetu.”
Baadhi ya wananchi wa Manispaa ya Morogoro walizungumza kwa kusema, wanaipongeza Takukuru kwa namna inavyookoa fedha za umma, kwani fedha hizo ni kwa manufaa ya wananchi walipakodi.
"Hii inatufanya tuendelee kuwa na Imani na Serikali yetu, kupitia TAKUKURU imekuwa ikiokoa fedha nyingi na miradi mingi Sasa inakamilika kwa wakati na thamani yake inaonekana,"alisema Khamis Mohamed mkazi wa Kihonda.
