Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
SERIKALI YALENGA SEKTA YA BIMA KUCHANGIA ASILIMIA 3 YA PATO LA TAIFA IFIKAPO 2030

SERIKALI YALENGA SEKTA YA BIMA KUCHANGIA ASILIMIA 3 YA PATO LA TAIFA IFIKAPO 2030

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Dodoma

SERIKALI imelenga kuongeza mchango wa sekta ya bima katika Pato la Taifa (GDP) kutoka asilimia 2.18 ya sasa hadi asilimia 3 ifikapo mwaka 2030, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuimarisha mchango wa sekta hiyo katika ukuaji wa uchumi wa nchi.

Hayo yalisemwa na Meneja wa Mipango na Utafiti wa Mamlaka ya Usimamizi wa Bima Tanzania (TIRA), Edgar Shao, aliyemwakilisha Kamishna wa Bima, Dkt. Baghayo Saqware, wakati wa uzinduzi wa ofisi ya mauzo ya Kampuni ya Bima ya Alliance jijini Dodoma.

Amesema sekta ya bima kwa sasa inachangia asilimia 2.18 ya Pato la Taifa, hatua inayoonyesha kuwa Tanzania ipo katika mwelekeo mzuri wa kufikia lengo la asilimia 3 ifikapo mwaka 2030.

Shao amesema kufikiwa kwa lengo hilo kutategemea ongezeko la wananchi wanaotumia huduma za bima, akibainisha kuwa bima husaidia kupunguza athari za kifedha zinazotokana na majanga na hatari mbalimbali, sambamba na kuimarisha uchumi wa mtu mmoja mmoja na taifa kwa ujumla.

Amewataka wananchi kujenga utamaduni wa kutumia huduma za bima ili kujilinda dhidi ya hasara zisizotarajiwa na wakati huo huo kuongeza mchango wa sekta hiyo katika maendeleo ya uchumi wa nchi.

Kwa upande wake, Mkuu wa Kitengo cha Bancassurance wa Kampuni ya Bima ya Alliance, Tumaini Pyanisa, alisema kufunguliwa kwa ofisi hiyo jijini Dodoma kutarahisisha upatikanaji wa huduma za bima kwa wananchi na kuongeza uelewa kuhusu umuhimu wa huduma hizo.

Amesema hatua hiyo ni sehemu ya mkakati wa kampuni wa kusogeza huduma karibu na wateja, kuongeza idadi ya wanufaika wa bima na kuchangia juhudi za Serikali za kukuza sekta ya bima nchini.

"TIRA imeendelea kusimamia sekta ya bima kwa kulinda maslahi ya wateja, kuimarisha utoaji wa huduma na kuweka mazingira yatakayowezesha sekta hiyo kufikia lengo la kuchangia asilimia 3 ya Pato la Taifa ifikapo mwaka 2030," Amesema.



 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3