CHAUMMA WAMPA BENSON KIGAILA KUKAIMU NAFASI YA KATIBU MKUU,SALIMU MWALIM ASIMAMISHWA
Na Matukio Daima Media
CHAMA cha Ukombozi wa Umma (CHAUMMA) kimemteua Benson Kigaila kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa chama hicho, akichukua nafasi ya Salum Mwalim baada ya Halmashauri Kuu ya chama kuamua kumvua madaraka.
Kwa mujibu wa taarifa kutoka chanzo cha kuaminika, uamuzi huo ulifikiwa usiku wa leo, Jumanne Juni 30, 2026, baada ya wajumbe wa Halmashauri Kuu kupiga kura ya kutokuwa na imani na Salum Mwalim, hatua iliyopelekea kuondolewa kwake katika nafasi hiyo.
Baada ya uamuzi huo, wajumbe walimuidhinisha kwa kauli moja Benson Kigaila, aliyekuwa Naibu Katibu Mkuu wa CHAUMMA Tanzania Bara, kuwa Kaimu Katibu Mkuu wa chama.
Mapema leo, Salum Mwalim alikuwa amemwandikia barua Mwenyekiti wa CHAUMMA, Hashim Rungwe, akieleza uamuzi wake wa kujiondoa kwa muda ili kupisha uchunguzi wa tuhuma zinazomkabili.
Hata hivyo, maamuzi ya Halmashauri Kuu yamekwenda mbali zaidi kwa kumwondoa rasmi Salum Mwalim katika nafasi ya Katibu Mkuu, na hivyo kumaliza uongozi wake ndani ya sekretarieti ya chama. Salum Mwalim pia alikuwa mgombea urais wa CHAUMMA katika Uchaguzi Mkuu wa Oktoba 2025.
