Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
SERIKALI YAANZA SAFARI YA KUIREJESHA HADHI YA PARETO KUPITIA MKAKATI MPYA WA MIAKA MITANO

SERIKALI YAANZA SAFARI YA KUIREJESHA HADHI YA PARETO KUPITIA MKAKATI MPYA WA MIAKA MITANO

 

Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media, Dodoma

Katika jitihada za kuifufua tasnia ya pareto na kuongeza mchango wake katika uchumi wa taifa, Serikali imezindua Mkakati wa Miaka Mitano (2026–2031) utakaolenga kuongeza uzalishaji, kuboresha ubora wa zao hilo na kuinua kipato cha wakulima.

Akifungua Mkutano Mkuu wa 16 wa Wadau wa Zao la Pareto jijini Dodoma kwa niaba ya Waziri wa Kilimo, Daniel Chingolo, Naibu Waziri wa Kilimo, David Silinde, alisema mkakati huo unakusudia kuongeza uzalishaji wa maua ya pareto kutoka tani 3,800 hadi tani 9,000 kwa mwaka ifikapo 2031.

Alisema serikali pia inalenga kuongeza tija ya uzalishaji kutoka wastani wa kilo 250–300 kwa hekta hadi kilo 800–1,200 kwa hekta, huku kiwango cha pyrethrin katika maua ya pareto kikiongezwa kutoka asilimia 1.3 hadi asilimia 2 ili kukidhi mahitaji ya soko la kimataifa.

Kwa mujibu wa Silinde, mkakati huo unahusisha usajili wa hekta 29,240 za mashamba ya pareto kupitia mfumo wa COPRA MIS, kuongeza uwezo wa usindikaji wa zao hilo kutoka asilimia 54 hadi asilimia 90, na kuongeza thamani ya mauzo ya nje kutoka dola za Marekani milioni 9 hadi milioni 15 kwa mwaka.

Aidha, serikali inalenga kuhakikisha wakulima wanapata kati ya asilimia 70 na 80 ya bei ya soko ili kuongeza motisha wa uzalishaji na kuboresha kipato chao.

Ili kufanikisha malengo hayo, serikali kwa kushirikiana na wadau mbalimbali itaimarisha uzalishaji wa mbegu bora kwa kushirikiana na TARI, PCT na PAITEC, ambapo kilo 15,000 za mbegu bora zinatarajiwa kuzalishwa.

Hatua nyingine zitakazotekelezwa ni pamoja na kuthibitisha aina mpya za mbegu zenye tija kubwa na kiwango cha juu cha pyrethrin, kutoa mafunzo kwa maafisa ugani 200 na wakulima 2,000 kuhusu kilimo bora cha pareto na elimu ya fedha, pamoja na kuboresha mifumo ya ukusanyaji wa taarifa za uzalishaji na biashara.

Mkakati huo pia unajumuisha ujenzi wa makaushio 129, uboreshaji wa vituo vya kukusanyia na kununulia pareto, na kuanzishwa kwa Mfuko wa Maendeleo ya Pareto kwa ajili ya kuimarisha tasnia hiyo kwa muda mrefu.

Silinde alisema utekelezaji wa mkakati huo katika mwaka wa kwanza utagharimu shilingi bilioni 2.2, fedha zitakazotolewa kwa ushirikiano kati ya serikali, sekta binafsi na wadau wengine wa mnyororo wa thamani wa zao hilo.

Alisisitiza kuwa serikali imejipanga kujenga tasnia ya pareto yenye ushindani katika soko la kimataifa na yenye manufaa makubwa kwa wakulima na wadau wengine.

Aidha, aliwataka wadau kutumia Mkutano Mkuu wa 16 wa Zao la Pareto kujadili changamoto na kutoa mapendekezo yatakayochochea ukuaji wa tasnia hiyo na kuongeza mchango wake katika maendeleo ya sekta ya kilimo na uchumi wa taifa.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3