Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
PURA YAELEZA MAFANIKIO YA SEKTA YA MAFUTA NA GESI, TANZANIA KUNUFAIKA ZAIDI NA RASILIMALI ZAKE

PURA YAELEZA MAFANIKIO YA SEKTA YA MAFUTA NA GESI, TANZANIA KUNUFAIKA ZAIDI NA RASILIMALI ZAKE


Na Ashrack Miraji 

Dodoma: Mamlaka ya Udhibiti wa Shughuli za Mkondo wa Juu wa Petroli Tanzania (PURA) imesema nchi inaendelea kunufaika kwa kiwango kikubwa na shughuli za utafutaji wa mafuta na gesi kupitia ongezeko la mapato ya serikali, ushiriki wa wazawa katika sekta hiyo pamoja na matumizi yanayoongezeka ya gesi asilia, hususan katika kampeni ya nishati safi ya kupikia inayotekelezwa na serikali.

Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma wakati wa kilele cha maadhimisho ya Wiki ya Utumishi wa Umma 2026, Mkurugenzi Mkuu wa PURA, , alisema mamlaka hiyo imepata mafanikio makubwa tangu kuanzishwa kwake kupitia usimamizi wa miradi ya utafutaji, uendelezaji na uzalishaji wa rasilimali za mafuta na gesi.

Sangweni alisema PURA inaendelea kuhakikisha mikataba yote inayosainiwa kati ya serikali na wawekezaji inaleta manufaa kwa taifa kupitia mirabaha, kodi na mapato mengine ya serikali, sambamba na kutoa fursa kwa Watanzania kupitia sera za ushiriki wa wazawa (Local Content).

“Tunafanya kila juhudi kuhakikisha miradi ya mafuta na gesi inaleta thamani kwa taifa huku ikitoa fursa za ajira, biashara na ushiriki wa wananchi katika sekta hii muhimu,” alisema.

Alieleza kuwa PURA inafuatilia kwa karibu utekelezaji wa sera na kanuni za ushiriki wa wazawa ili kuhakikisha kampuni na wataalamu wa Kitanzania wananufaika na fursa zinazotokana na sekta hiyo pale uwezo wa ndani unapopatikana.

Aidha, alisema zabuni za bidhaa na huduma zinazopatikana nchini zinaendelea kupewa kipaumbele kwa kampuni za Kitanzania, huku juhudi zikifanyika kuwawezesha wataalamu wa ndani kufikia viwango vya kimataifa vinavyohitajika katika sekta ya mafuta na gesi.

Kwa upande mwingine, PURA imebainisha kuwa kampeni ya matumizi ya nishati safi ya kupikia inayoongozwa na Rais imechochea ongezeko la matumizi ya gesi asilia kama mbadala wa nishati za jadi za kupikia, jambo ambalo limeongeza mahitaji ya rasilimali za nishati zinazozalishwa nchini.

Sangweni alisema matumizi yanayoongezeka ya gesi asilia katika kaya na taasisi mbalimbali yameimarisha dhamira ya PURA ya kuendelea kuunga mkono maendeleo ya rasilimali za gesi ili ziweze kuchangia ukuaji wa uchumi wa taifa.

“Tanzania ina rasilimali kubwa za gesi asilia na mahitaji yake yanaendelea kuongezeka. Rasilimali hii ina nafasi muhimu katika kuchochea maendeleo na kuharakisha mpito kuelekea matumizi ya nishati safi,” alisema.

Aliongeza kuwa sekta ya mafuta na gesi nchini inaendelea kuwekeza nguvu katika shughuli za utafutaji wa rasilimali hizo, huku matarajio yakiendelea kuwepo ya kugunduliwa kwa mafuta yenye tija ya kibiashara pamoja na hifadhi za gesi asilia ambazo tayari zimethibitishwa.

Kwa mujibu wa Sangweni, mwelekeo wa dunia katika matumizi ya nishati unaendelea kubadilika kutokana na kuongezeka kwa matumizi ya magari ya umeme na nishati mbadala, lakini gesi asilia itaendelea kuwa nishati muhimu ya mpito kwa mataifa mengi, ikiwemo Tanzania.

PURA ina jukumu la kusimamia na kudhibiti shughuli zote za mkondo wa juu wa petroli, zikiwemo utafutaji, tathmini, uendelezaji na uzalishaji wa mafuta na gesi, huku ikihakikisha shughuli hizo zinafanyika kwa kuzingatia sheria, mikataba na sera za taifa.

Mamlaka hiyo imesisitiza kuwa lengo lake la muda mrefu ni kuhakikisha rasilimali za mafuta na gesi za Tanzania zinachangia kikamilifu katika mageuzi ya uchumi, usalama wa nishati na maendeleo endelevu ya nchi.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3