Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
POLISI MWANZA WAANZA UKAGUZI WA MAGARI YA SHULE KUIMARISHA USALAMA WA WANAFUNZI

POLISI MWANZA WAANZA UKAGUZI WA MAGARI YA SHULE KUIMARISHA USALAMA WA WANAFUNZI

NA CHAUSIKU SAID 
MATUKIO DAIMA MWANZA.

MWANZA, Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza limeanza zoezi la ukaguzi wa magari yanayobeba wanafunzi kwa lengo la kuhakikisha yanakuwa salama na yenye ubora wa kuwahudumia wanafunzi wakati wote.

Akifungua zoezi hilo Juni 18, 2026, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza, Wilbroad Mutafungwa, alisema kifungu cha 45 cha Sheria ya Usalama Barabarani Sura ya 168 iliyorekebishwa mwaka 2023 kinaelekeza kufanyika kwa ukaguzi wa magari ya shule, huku kikibainisha wajibu wa wamiliki wa magari na Jeshi la Polisi kuhakikisha vyombo hivyo vinakuwa katika hali ya usalama.

Ameeleza kuwa  magari yatakayobainika kuwa na kasoro yatatakiwa kufanyiwa marekebisho na kurejeshwa kwa ukaguzi kabla ya kuruhusiwa kuendelea kutoa huduma, na kubainisha kuwa ongezeko la shule na magari ya wanafunzi Mkoani Mwanza linaifanya kazi hiyo kuwa muhimu ili kuhakikisha wanafunzi wanafika na kurejea nyumbani kwa usalama.


Kamanda Mutafungwa alisema serikali imeweka mkazo katika kuhakikisha wanafunzi wanapata elimu bora katika mazingira salama, ikiwemo usafiri wa uhakika, hivyo magari yote yanapaswa kukidhi viwango vinavyotakiwa.

Katika ukaguzi huo, magari yatapimwa ubora wake,  pamoja na rangi maalum ya njano kwa magari ya shule, pamoja na uhalali wa nyaraka muhimu kama bima, leseni za usafirishaji zinazotolewa na LATRA na leseni za madereva kulingana na madaraja yanayoruhusiwa.

Aidha, alisema ukaguzi unahusisha wahudumu wa magari ya shule (matroni na patroni) ambao wana jukumu la kusimamia usalama wa watoto, hasa kutokana na ongezeko la matukio ya ukatili dhidi ya watoto wakati wa usafiri.

Kamanda Mutafungwa alitaja baadhi ya changamoto zinazojitokeza kuwa ni baadhi ya wamiliki wa shule kutofikisha magari yao kwa ukaguzi, kuficha ubovu wa magari, kukosekana kwa matroni na patroni, kujaza wanafunzi kupita uwezo wa gari na matumizi ya magari yasiyoruhusiwa kusafirisha wanafunzi.


Kwa upande wake, Mkuu wa kikosi cha Usalama Barabarani Mkoa wa Mwanza, Sunday Ibrahim  ameleema zoezi hilo linalenga kubaini ubora wa magari na uhalali wa madereva pamoja na kutoa elimu ya usalama barabarani kwa madereva na wahudumu wa magari hayo.


Alisema mwaka 2025 jumla ya shule 173 na magari 297 yalifanyiwa ukaguzi, ambapo magari 27 yalibainika kuwa na kasoro mbalimbali na kutakiwa kufanyiwa marekebisho. Mwaka 2024, shule 147 na magari 271 yalikaguliwa, huku magari 39 yakibainika kuwa na hitilafu ndogo ndogo.

Naye mwakilishi wa madereva wa magari ya shule, Baraka Daud, aliomba ukaguzi huo uwe wa mara kwa mara ili kusaidia kupunguza ajali na kuimarisha usalama wa wanafunzi.

Kwa upande wake, mhudumu wa magari ya shule (matroni), Betha Nicholaus, alisema matroni na patroni wanapaswa kutekeleza majukumu yao kwa uadilifu na kuhakikisha watoto wanakuwa salama wanapotolewa nyumbani hadi wanaporejeshwa.

"Jukumu letu ni kuhakikisha watoto wanakuwa salama wakati wote wa safari. Tunapaswa kuwahudumia kwa upendo na kuwalinda kama watoto wetu wenyewe," alisema Betha.




 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3