Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MATUMIZI YA MODULI YA KIELEKTRONIKI YARAHISISHA USULUHISHI WA MIGOGORO YA ZABUNI

MATUMIZI YA MODULI YA KIELEKTRONIKI YARAHISISHA USULUHISHI WA MIGOGORO YA ZABUNI

 



Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma

MAMLAKA  ya Rufani ya Zabuni za Umma (PPAA) imesema matumizi ya moduli ya kushughulikia malalamiko na rufaa kwa njia ya kielektroniki yameleta mageuzi makubwa katika usimamizi wa migogoro ya ununuzi wa umma kwa kuongeza kasi, uwazi na ufanisi wa utoaji wa maamuzi.


Akizungumza alipotembelea banda la PPAA katika maonesho ya Wiki ya Utumishi wa Umma yanayoendelea katika Viwanja vya Chinangali Grounds jijini Dodoma, Katibu Mtendaji wa mamlaka hiyo, James Sando, alisema moduli hiyo inayopatikana kupitia Mfumo wa Ununuzi wa Umma wa Tanzania (NeST) imeondoa changamoto nyingi zilizokuwa zikikwamisha utatuzi wa migogoro ya zabuni.

Amesema kabla ya kuanzishwa kwa mfumo huo, wadau walikabiliwa na changamoto za ucheleweshaji wa nyaraka, gharama za uwasilishaji pamoja na ugumu wa kufuatilia mwenendo wa mashauri yaliyowasilishwa.


Kwa mujibu wa Sando, matumizi ya teknolojia hiyo yamewezesha taasisi nunuzi na wazabuni kuwasilisha na kufuatilia malalamiko yao kwa urahisi zaidi huku yakihakikisha kumbukumbu zote muhimu zinatunzwa kwa usahihi.

“Leo hii tunapata nyaraka na taarifa zinazohitajika kwa wakati, jambo linalotusaidia kufanya uchambuzi na kutoa maamuzi kwa haraka zaidi mfumo huu umeongeza uwazi na kurahisisha mawasiliano kati ya PPAA na taasisi nunuzi,” amesema.

Ameeleza kuwa katika mwaka wa fedha 2025/26, jumla ya malalamiko 157 yamewasilishwa kupitia moduli hiyo kwa taasisi nunuzi, huku mashauri 37 yakifikishwa PPAA kwa ajili ya rufaa na kufanyiwa maamuzi.

Sando amesema takwimu hizo zinaonesha kuwa wadau wa ununuzi wa umma wameendelea kuamini na kutumia mfumo huo, ambao umekuwa nyenzo muhimu katika kuimarisha usimamizi wa haki katika michakato ya zabuni.


Aidha, amesema PPAA inaendelea kuboresha huduma zake za kidijitali na ina mpango wa kuunganisha mfumo huo na mfumo wa utoaji haki wa Mahakama ya Tanzania katika mwaka wa fedha ujao ili kurahisisha zaidi upatikanaji wa haki na kuimarisha uwajibikaji katika sekta ya ununuzi wa umma.


Ameongeza kuwa hatua hiyo itasaidia kuunda mfumo jumuishi wa usimamizi wa mashauri ya ununuzi wa umma kuanzia ngazi za awali za malalamiko hadi hatua za mwisho za utoaji wa haki.


Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3