Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
MAPITIO YA SERA YATAKIWA KUIMARISHA HUDUMA KWA WALEMAVU

MAPITIO YA SERA YATAKIWA KUIMARISHA HUDUMA KWA WALEMAVU

Matukio Daima, Morogoro

WADAU wa masuala ya watu wenye ulemavu wameitaka Serikali kuimarisha sera, sheria na miongozo mbalimbali ili kuboresha huduma za usaidizi kwa watu wenye ulemavu na kutambua mchango wa watu wanaowahudumia.

Wito huo unatolewa mjini Morogoro wakati wa mkutano wa wadau unaojadili ripoti ya uchambuzi wa sera uliofanywa kupitia Mradi wa Kutetea Haki za Watu Wenye Ulemavu katika Kuimarisha Sera, Sheria na Mipango Inayohusu Watoa Huduma za Malipo na Zisizo za Malipo kwa Watu Wenye Ulemavu (UNPRPD), unaosimamiwa na Shirika la Maendeleo la Umoja wa Mataifa (UNDP).

Mratibu wa Mradi wa UNPRPD kutoka UNDP, Ghati Horombe, amesema mradi huo unaotekelezwa kwa kipindi cha miaka miwili unalenga kujenga uelewa kwa wadau mbalimbali kuhusu haki na mchango wa watu wanaotoa huduma za malipo na zisizo za malipo kwa watu wenye ulemavu.

Amesema kupitia mradi huo, wadau kutoka wizara mbalimbali, taasisi za umma, mashirika ya watu wenye ulemavu na asasi za kiraia wanapatiwa mafunzo na kushirikishwa katika mijadala ya kisera ili kuongeza uelewa kuhusu kundi hilo na umuhimu wa kulitambua.

Horombe anasema mradi huo pia unafanya uchambuzi wa kina wa sera mbalimbali ikiwemo sera ya watu wenye ulemavu, afya, jinsia, maji na nyaraka nyingine za kisera ili kubaini namna masuala ya watoa huduma kwa watu wenye ulemavu yanavyozingatiwa katika mipango na mikakati ya taifa.

Ameongeza kuwa matokeo ya uchambuzi huo yanaonyesha maeneo ambayo Sera zimefanikiwa pamoja na maeneo yanayohitaji maboresho, huku wadau wakikutana kujadili mapendekezo yatakayosaidia kuimarisha mfumo wa utoaji huduma na uangalizi kwa watu wenye ulemavu nchini.

Katibu Mkuu wa Shirikisho la Vyama vya Watu Wenye Ulemavu Tanzania (SHIVYAWATA), Jonas Lubago, amesema wadau wanapitia uchambuzi wa sera 32 za umma kutoka wizara mbalimbali ili kuona namna zinavyozungumzia huduma, malezi na usaidizi kwa watu wenye ulemavu.

Amesema pamoja na hatua mbalimbali zilizochukuliwa na Serikali kuboresha maisha ya watu wenye ulemavu, bado kuna maeneo yanayoonyesha mapungufu hususan katika utambuzi wa watu wanaowahudumia.

Kwa mujibu wa Lubago, uchambuzi huo unaonyesha kuwa baadhi ya sera hazijaweka wazi namna watu wanaowasaidia watu wenye ulemavu wanavyotambuliwa, wanavyowezeshwa au kufidiwa kwa muda wanaoutumia kutoa huduma hizo.

Amesema changamoto hiyo inaonekana zaidi kwa wanawake ambao mara nyingi hubeba jukumu kubwa la kuwahudumia watu wenye ulemavu majumbani na hivyo kushindwa kushiriki kikamilifu katika shughuli nyingine za uzalishaji mali.

Lubago amesema kutokana na hali hiyo ipo haja ya Serikali kuangalia uwezekano wa kuhuisha sera zilizopo au kuweka mifumo itakayosaidia kutambua na kuwezesha watu wanaotoa huduma kwa watu wenye ulemavu.

Aidha amesema eneo hilo lina fursa kubwa ya kiuchumi na linaweza kuzalisha ajira nyingi zaidi ikiwa litapewa nafasi stahiki katika sera, sheria na miongozo mbalimbali ya maendeleo.

Kwa upande wake, Mkurugenzi Mtendaji wa Chama cha Viziwi Tanzania (CHAVITA), Dickson Mveyange, amesema Tanzania ina sera nyingi zenye maelekezo mazuri lakini changamoto kubwa inaendelea kuwa utekelezaji wake.

Amebainisha kuwa baadhi ya sera zilizopo zinaendana na mahitaji ya watu wenye ulemavu huku nyingine zikihitaji kufanyiwa maboresho ili kuendana na mabadiliko ya kijamii na kiuchumi yanayoendelea kutokea.

Mveyange amesema upungufu wa rasilimali za kutosha ni miongoni mwa sababu zinazochangia baadhi ya sera kushindwa kuleta matokeo yaliyokusudiwa kwa walengwa.

Ameitaka Serikali kufanya tathmini ya mara kwa mara ya sera zilizopo ili kubaini maeneo yanayohitaji maboresho na kuongeza uwekezaji katika utekelezaji wake kwa manufaa ya wananchi na hasa watu wenye ulemavu.

Naye Afisa Ufuatiliaji na Tafiti wa Taasisi ya Wasioona Tanzania (TAB), Bernad Kindoli, amesema Tanzania imepiga hatua kubwa katika kuandaa sera na sheria zinazolinda haki za watu wenye ulemavu pamoja na makundi mengine maalumu katika jamii.

Amesema lengo la mapitio yanayofanyika sasa siyo kuonyesha kuwa hakuna mafanikio yaliyopatikana, bali kubaini maeneo yanayoweza kuboreshwa zaidi ili huduma za usaidizi ziwe bora na ziwasaidie watu wenye ulemavu kujitegemea.

Kindoli amesema wadau wanataka kuona sera na sheria zinaendelea kutambua na kuthamini shughuli za usaidizi, huku upatikanaji wa rasilimali za kutosha ukizingatiwa ili kuongeza ufanisi wa huduma hizo.

Amefafanua kuwa hatua hizo zitasaidia kupunguza mzigo kwa familia na walezi, kuongeza uwezo wa watu wenye ulemavu kujitegemea na kuhakikisha sauti za wanaohitaji huduma za usaidizi zinasikika katika mchakato wa maamuzi.


Mwisho

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3