PROF SHEMDOE-SERIKALI KUENDELEA KUIMARISHA MIUNDOMBINU YA MICHEZO NCHINI.
NA MATUKIO DAIMA MEDIA.
IRINGA.Waziri wa nchi Ofisi ya Waziri Mkuu-TAMISEMI Mhe. Prof.Riziki Shemdoe, amesema kuwa Serikali ya Tanzania itaendelea kuimarisha miundombinu ya michezo nchini, ili kuendelea kukuza sekta hiyo.
Prof.Shemdoe amesema hayo leo Juni,2026 Mjini Iringa, wakati akizungumza katika ufunguzi wa Mashindano ya UMITASHUMTA na UMISSETA yanayofanyika Kitaifa Mkoani humo.
Amesema kuwa lengo la kuimarisha miundombinu ni kuhakikisha kuwa vipaji vinavyoibuliwa havipotei, na vinaendelezwa kwa ajili ya kuja kulitumikia Taifa kupitia timu mbalimbali za ndani na nje ya nchi.
"Serikali itaendelea kuhakikisha kuwa michezo na Sanaa inapewa kipaumbele katika shule, kwa michezo ni uchumi iwapo itawekeza msingi mzuri" amesisitiza Prof.Shemdoe.
Sambamba na hilo, serikali imeelekeza halmashauri zote nchini kuanzisha shule maalumu za kukuza vipaji na kutenga fedha za maendeleo ya michezo na sanaa, ikiwa ni sehemu ya jitihada za kuifanya sekta hiyo kuwa chachu ya ajira, afya bora na maendeleo ya uchumi.
“Michezo na sanaa zimekuwa sekta muhimu zinazoweza kuibua vipaji, kuzalisha ajira na kuwajengea vijana uwezo wa kushindana katika soko la ajira la ndani na nje ya nchi”
Aidha kaulimbiu ya mwaka huu inayosema "Michezo na Sanaa Shuleni; Daraja la Ajira, Afya na Ushindani wa Kimataifa" inaakisi dhamira ya serikali ya kutumia michezo na sanaa kama nyenzo ya maendeleo ya kijamii na kiuchumi.
Awali akitoa salam za Mkoa, Mkuu wa Mkoa wa Iringa Kheri James alisema kuwa mashindano hayo ni fursa kwa wananchi ambao watapata nafasi ya kufanya shughuli mbalimbali za kiuchumi.
Alisema Mkoa huo umejipanga kwa ajili ya kuwahudumia wageni zaidi ya elfu 10 watakaohusika katika mashindano ya mwaka huu.
"Wananchi wa Iringa tumepewa heshima hii ya kuandaa mashindano hayo tangu mwaka jana, tunawahakikishia kuwa huduma zote muhimu zinapatikana wakati wowote hivyo wageni wote waendelee kufurahia michezo inayoendelea" alisema
MWISHO.