KIBANO KINAKUJA KWA WAFANYABIASHARA MANISPAA YA WANAOTUMIA VIPAZA SAUTI NA SPIKA ZA MIZIKI KUTANGAZA BILA VIBALI
NA MATUKIO DAIMA MEDIA,
Halmashauri ya Manispaa ya Iringa imesema imejipanga kuanza msako mkali dhidi ya matumizi holela ya vipaza sauti na muziki katika maeneo ya biashara.
Kuwa hatua hiyo inakuja kufuatia malalamiko ya wananchi kuhusu kelele zinazotokana na matangazo ya biashara katika maeneo mbalimbali ya mji huo.
Kauli hiyo ilitolewa na Afisa Utamaduni na Michezo na sanaa wa Manispaa ya Iringa, Dkt. Carlos Minda,kwa niaba ya aliyemwakilisha Mkurugenzi wa Halmashauri ya Manispaa ya IringaZainab Mlawa.
Dkt Minda alisema matangazo yote yanayohusisha matumizi ya muziki au vipaza sauti katika maeneo ya umma yanapaswa kufuata taratibu na kupata vibali kutoka mamlaka husika.
Alieleza kuwa vibali vinavyotolewa huambatana na masharti maalumu yanayowataka waombaji kupunguza sauti wanapopita au wanapokuwa karibu na maeneo yanayohitaji utulivu kama vile hospitali, mahakama, makanisa, misikiti na ofisi mbalimbali.
“Vibali tunavyotoa vinaelekeza wazi maeneo ambayo yanahitaji utulivu,mtu anapofanya matangazo anatakiwa kuzingatia masharti hayo ili kuepusha usumbufu kwa wananchi,” alisema.
Aidha, alisema wafanyabiashara wanaoweka vipaza sauti au redio zenye sauti kubwa mbele ya maduka yao kwa lengo la kuvutia wateja wanakiuka taratibu zilizowekwa, kwani leseni wanazopewa ni za kufanya biashara na si za kufanya matangazo ya sauti bila kibali maalumu.
Kwa mujibu wa afisa huyo, manispaa kwa kushirikiana na idara za biashara na mazingira ilifanya zoezi la sensa kubaini wafanyabiashara wanaotumia vipaza sauti katika maeneo yao ya biashara na tayari baadhi yao walipewa barua za kusitisha shughuli hizo.
“Tumeshachukua hatua za awali kwa kutoa elimu na taarifa kwa wahusika. Lengo letu si kuwaadhibu wafanyabiashara bali kuhakikisha shughuli za biashara zinafanyika kwa kuzingatia sheria na kulinda utulivu wa wananchi,” alisema.
Dkt. Minda aliongeza kuwa matumizi ya vipaza sauti bila utaratibu yanaweza kuwa chanzo cha usumbufu wa mazingira na hivyo ni muhimu kwa kila mfanyabiashara kuzingatia sheria zilizopo.
Wananchi wa Iringa wamekuwa wakitoa malalamiko kuhusu kelele za muziki na matangazo ya biashara katika baadhi ya maeneo ya mji huo, wakidai hali hiyo inaathiri utulivu wa mazingira pamoja na shughuli za kila siku.
Halmashauri imewahimiza wananchi kuendelea kutoa taarifa pale wanapoona ukiukwaji wa taratibu ili hatua stahiki ziweze kuchukuliwa kwa mujibu wa sheria.
Baadhi ya wakazi wa Manispaa ya Iringa wameeleza wasiwasi wao kuhusu ongezeko la kelele zinazotokana na redio zinazopigwa kwa sauti kubwa katika maduka pamoja na pikipiki zinazotoa kelele nyingi, wakisema hali hiyo inaathiri utulivu na usalama wa wananchi.
Akizungumza mjini Iringa, mkazi mmoja wa eneo hilo, Mchungaji Gaitan Msemwa, alisema kila mwananchi ana haki ya kufanya kazi na kuendesha biashara zake, lakini ni muhimu shughuli hizo zikafanyika kwa kuzingatia ustawi wa jamii na kuheshimu haki za wengine.
Alisema baadhi ya wafanyabiashara huweka redio zenye sauti kubwa mbele ya maduka yao kwa lengo la kuvutia wateja, jambo ambalo kwa upande mwingine husababisha usumbufu kwa wananchi wanaopita au wanaofanya shughuli zao katika maeneo hayo.
“Watu wengi wanapitia changamoto mbalimbali za maisha. Wengine wana mawazo, wengine ni wazee wanaohitaji utulivu. Kelele kubwa za redio zinaweza kuwa kero kwao,” alisema.
Aidha, alieleza kuwa kelele hizo zinaweza kuhatarisha usalama wa watumiaji wa barabara kwa sababu wakati mwingine mtu hushindwa kusikia honi za vyombo vya usafiri vinavyopita karibu naye kutokana na sauti kubwa za muziki.
Mbali na redio za madukani, mkazi huyo pia aligusia tatizo la pikipiki zinazotoa kelele nyingi, akisema baadhi ya waendesha pikipiki wamekuwa wakitumia vyombo vyao bila kuzingatia viwango vinavyokubalika vya sauti.
Mcungaji Gaitan alitoa wito kwa wafanyabiashara na waendesha pikipiki kuzingatia matumizi ya sauti za wastani ili kulinda afya, utulivu na usalama wa wananchi.
“Biashara zifanyike, lakini zifanyike kwa namna ambayo haitaleta usumbufu kwa wengine. Redio ziwekwe kwa sauti za kawaida na pikipiki zitunzwe ili zisitoe kelele zisizo za lazima,” alisema.
Kwa upande wao wakazi wengine wa Iringa wameendelea kusisitiza umuhimu wa mamlaka husika kuelimisha jamii kuhusu athari za uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele, ili kuhakikisha mji unaendelea kuwa sehemu salama na yenye mazingira mazuri kwa wote.
Baadhi yao wameiomba serikali na mamlaka za mji huo kuweka utaratibu madhubuti wa kudhibiti kelele zinazotokana na matangazo ya biashara yanayofanywa kupitia vipaza sauti katika maeneo mbalimbali ya biashara.
Wakizungumza katika mahojiano tofauti, wananchi hao walisema matumizi holela ya spika na matangazo ya sauti kubwa yamekuwa chanzo cha uchafuzi wa mazingira na usumbufu kwa wakazi wa mji huo.
Mkazi wa Iringa, Ponsiane Kayage, alisema serikali inapaswa kuweka sheria na taratibu zitakazowataka wafanyabiashara wanaotumia vipaza sauti kupata vibali maalumu na kulipia huduma hiyo ili kuchangia mapato ya serikali.
“Wale wanaotaka kutumia vipaza sauti kwa ajili ya matangazo waombe vibali rasmi. Hii itasaidia kuongeza mapato ya serikali na wakati huo huo kudhibiti matumizi holela ya vifaa hivyo,” alisema.
Aliongeza kuwa wafanyabiashara wanaofanya matangazo bila vibali wanapaswa kuchukuliwa hatua za kisheria ili kuondoa usumbufu unaowakabili wananchi kila siku.
Naye mkazi mwingine wa Manispaa ya Iringa alisema kelele za spika zimekuwa kero kwa watu wanaopita katika maeneo ya biashara, kwani karibu kila duka lina mfumo wake wa matangazo unaotoa sauti kubwa kwa wakati mmoja.
“Unapita katika eneo la biashara unakutana na spika kila baada ya hatua chache. Hali hii inaleta usumbufu mkubwa kwa wananchi na wageni wanaotembelea mji wetu,” alisema.
Wananchi hao walieleza kuwa Iringa ni moja ya lango muhimu la utalii katika Ukanda wa Nyanda za Juu Kusini, hivyo ni muhimu kuhakikisha mazingira ya mji yanabaki safi, tulivu na rafiki kwa wageni na watalii.
Walisema hatua za kudhibiti matumizi ya vipaza sauti zinaweza kusaidia kuboresha taswira ya mji na kuongeza ustaarabu katika shughuli za biashara.
Baadhi yao walipendekeza mfumo wa utoaji vibali na ushuru maalumu kwa watumiaji wa vipaza sauti, wakisema utaratibu huo unaweza kusaidia kupunguza kelele zisizo za lazima huku ukiiongezea serikali mapato.
Maoni hayo yanakuja wakati Manispaa ya Iringa ikiendelea kutafuta njia za kudhibiti uchafuzi wa mazingira unaotokana na kelele za matangazo ya biashara na matumizi yasiyo rasmi ya vipaza sauti katika maeneo ya umma.
SHERIA YA NEMC
Baraza la Taifa la Hifadhi na Usimamizi wa Mazingira (NEMC) limeendelea kuhimiza wananchi, taasisi na wafanyabiashara kuzingatia sheria na kanuni za udhibiti wa kelele na mitetemo ili kulinda afya za wananchi na mazingira.
Kelele ni Nini?
Kwa tafsiri ya kawaida, kelele ni sauti kubwa, isiyohitajika na ya kuudhi ambayo husababisha kero au hisia zisizofurahisha kwa anayeisikia.
Kwa mujibu wa Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya mwaka 2004, Kifungu cha 3, kelele ni aina ya uchafuzi wa mazingira unaotokana na sauti ambayo kwa asili yake inakataliwa au inaweza kusababisha madhara kwa afya ya binadamu, viumbe hai na mazingira.
Pia, ni sauti yoyote inayoweza kutambuliwa na Kamati ya Taifa ya Viwango vya Mazingira kuwa ni kelele.
Athari za Kelele
Kelele zinazozidi viwango vinavyoruhusiwa zinaweza kusababisha madhara mbalimbali, yakiwemo:
Kupoteza au kudhoofika kwa uwezo wa kusikia.
Kukosa usingizi.
Msongo wa mawazo na usumbufu wa kisaikolojia.
Kuvuruga mawasiliano kati ya watu.
Kupungua kwa ufanisi wa kazi na shughuli za kila siku.
Vyanzo Vikuu vya Kelele
Kelele chafuzi hutokana na shughuli mbalimbali za kibinadamu, zikiwemo:
Ujenzi wa majengo na miundombinu.
Kumbi za starehe na burudani.
Viwanda na shughuli za uzalishaji.
Nyumba za ibada.
Vyombo vya usafiri.
Magari ya matangazo na shughuli nyingine zinazotumia vifaa vya sauti.
Njia za Kudhibiti Kelele
NEMC inapendekeza hatua zifuatazo ili kudhibiti kelele zinazozidi viwango:
Wamiliki wa kumbi za starehe na burudani kutumia vifaa vya kuzuia kelele (soundproofing) pamoja na vipima kelele (sound meters).
Wafanyabiashara kuhakikisha wanapata vibali vinavyotakiwa kutoka mamlaka husika na kuzingatia masharti ya uendeshaji wa shughuli zao.
Kuzingatia matumizi sahihi ya ardhi kabla ya kuanzisha shughuli zinazoweza kuzalisha kelele nyingi.
Sheria na Kanuni Zinazosimamia Kelele
Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ya Mwaka 2004
Kifungu cha 106(5) kinaeleza kuwa:
"Hairuhusiwi kwa mtu yeyote kupiga kelele au kusababisha kelele kuzidi kiwango kilichowekwa au kitakachowekwa kwa mujibu wa sheria."
Aidha, Kifungu cha 106(6) kinaainisha kuwa ni kosa kwa mtu yeyote kusababisha uchafuzi wa mazingira kwa kelele bila kuzingatia taratibu na njia bora zilizoainishwa katika kanuni husika.
Kanuni za Usimamizi wa Mazingira za Viwango vya Udhibiti wa Kelele na Mitetemo za Mwaka 2015
Kanuni hizi zilitungwa chini ya Sheria ya Usimamizi wa Mazingira ili:
Kulinda afya ya binadamu na mazingira dhidi ya madhara ya kelele na mitetemo.
Kuweka viwango vya juu vinavyoruhusiwa vya kelele katika maeneo mbalimbali.
Kuelekeza namna bora ya kudhibiti na kuzuia athari za kelele na mitetemo.
Viwango vya Kelele Vinavyoruhusiwa
Kwa mujibu wa Kanuni za mwaka 2015, viwango vya juu vya kelele vinavyoruhusiwa ni:
Mchana
Usiku
Viwandani
85 dBA
65 dBA
Makazi yaliyochanganyika na biashara/burudani
55 dBA
45 dBA
Makazi yenye viwanda vidogo
65 dBA
50 dBA
Maeneo ya biashara
75 dBA
50 dBA
Hospitali, taasisi za elimu, kumbi za mikutano, makazi ya wazee na maeneo ya mapumziko 45 dBA,35 dBA
NEMC inatoa wito kwa wananchi, taasisi, waendeshaji wa biashara na wadau wote wa maendeleo kuhakikisha wanazingatia sheria na kanuni za udhibiti wa kelele. Hatua hii itasaidia kulinda afya za wananchi, kuboresha mazingira ya kazi na makazi, pamoja na kuhakikisha mazingira safi na salama kwa vizazi vya sasa na vijavyo

