HIFADHI YA TAIFA YA ARUSHA NA UPEEKE WA VIVUTIO.
Na,Jusline Marco:Arusha
Hifadhi ya Taifa Arusha ni miongoni mwa hifadhi 21 zilizopo nchini pia ni hifadhi ukongwe iliyoanzishwa mwaka 1960 ikiwa na umbali wa kilometa 30 kutoka jijini Arusha, ikitanguliwa na hifadhi ya Taifa Serengeti Kisha kufuatiwa na hifadhi ya Taifa ya Ziwa Manyara.
Katika hifadhi hiyo vipo vivutio mbalimbali ikiwemo wanyamapori,Mlima Meru,ndege aina ya flamingo,mbega,maziwa ya momela,kasoko ya ngurudoto(Creta), pamoja na Mkuyu wenye pango, unaojulikana kama Fig Tree Arch,ambao ni moja ya vivutio vya kipekee vinavyopatikana ndani ya hifadhi ya Arusha.
Mti huu mkubwa wa mkuyu umeunda upinde wa asili katikati yake kiasi kwamba gari la watalii linaweza kupita chini yake, hii imeufanya kuwa kivutio maarufu kwa wapenda mazingira na wapiga picha.
Mkuyu huu ulitokea kwa mchakato wa asili ambapo mbegu za mkuyu zilidondoshwa na ndege juu ya mti mwingine ambapo kadiri mkuyu ulivyokua, mizizi yake ilishuka kuelekea ardhini na kuuzunguka mti uliokuwa mwenyeji wake hadi ukafa Kisha baada ya muda, kilichobaki ni muundo wa mizizi na shina uliounda pango au upinde mkubwa unaoonekana leo.
Mkuyu wenye pango upo kwenye eneo la misitu ya mlimani kwenye miteremko ya Mount Meru, eneo ambalo lina miti mingi ya mikuyu, tumbili aina ya colobus, na ndege mbalimbali ambapo Watalii wengi husimama hapo na kupiga picha na kufurahia mandhari ya kipekee ya mti huu wa kihistoria.
Afisa Mwandamizi wa Uhifadhi kitengo cha Utalii hifadhi ya Taifa Arusha Jerome Boniface Ndanzi amesema kugundulika kwa mti huo wa pili kutaongeza upekee wa hifadhi hiyo kwani ni miti pekee ambayo hupatikana ndani ya hifadhi ya Taifa Arusha.
Amesema Mbali na uzuri wake, mkuyu huo ni mfano mzuri wa jinsi mazingira ya asili yanavyoweza kuunda maumbo ya ajabu bila kuingiliwa na binadamu, leo hii Mkuyu wenye Pango ni moja ya alama zinazotambulisha Hifadhi ya Taifa ya Arusha na huvutia wageni kutoka sehemu mbalimbali duniani.
Kwa ufupi Mkuyu wenye Pango ni kivutio maarufu cha utalii katika Hifadhi ya Taifa ya Arusha na ni mfano wa kipekee wa maajabu ya mazingira ya Tanzania ambapo hivi karibuni mkuyu mwingine umegundulika katika hifadhi hiyo na kuzidi kupitia watalii wengi zaidi.


