CCM YAONYA KUHUSU MIKUTANO INAYODAIWA KUCHOCHEA MAAANDAMANO, YATOA WITO WA KULINDA AMANI
Jun 13, 2026
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
CHAMA Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kinazo taarifa zinazoashiria kuwepo kwa mikutano inayofanywa na baadhi ya viongozi wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA), ambayo inadaiwa kuhusisha mipango ya kuhamasisha maandamano yenye uwezekano wa kuvuruga hali ya amani nchini.
Akizungumza na waandishi wa habari jijini Dodoma, Katibu wa Halmashauri Kuu ya Taifa (NEC) wa CCM anayeshughulikia Itikadi, Uenezi na Mafunzo, Kenani Kihongosi, alisema chama hicho kimeendelea kuwataka Watanzania kuzingatia umuhimu wa utulivu na mshikamano wa kitaifa.
Kihongosi ameeleza kuwa CCM inaamini maendeleo endelevu hayawezi kupatikana iwapo kutakuwa na misukosuko ya kisiasa, akisisitiza kuwa tofauti za vyama zinapaswa kuishia kwenye majadiliano ya sera.
Alisema chama hicho kinatoa tahadhari kwa wananchi kutoshawishika kushiriki katika matukio yanayoweza kusababisha machafuko, akibainisha kuwa amani ndiyo msingi wa maendeleo ya taifa.
“Taarifa tulizonazo zinaonyesha kuwepo kwa vikao vinavyohusisha maandalizi ya maandamano ambayo yanaweza kuhatarisha utulivu wa nchi tunawasihi wananchi wasishiriki mambo ya aina hiyo,” amesema Kihongosi.
Aidha, amebainisha kuwa vyombo vya usalama vina wajibu wa kuendelea kulinda utulivu wa nchi na kuhakikisha raia na mali zao wapo salama wakati wote.
Kihongosi amewahimiza vijana kutumia nguvu zao katika shughuli za kiuchumi na maendeleo badala ya kujiingiza katika vitendo vinavyoweza kuleta taharuki au migogoro.
Amesema pia ni muhimu kwa wananchi kutoa taarifa kwa mamlaka husika wanapoona viashiria vya vitendo vinavyoweza kuhatarisha amani ya nchi.
Akizungumzia maandamano kwa ujumla, alisema mara nyingi madhara yake huwakumba wananchi wa kawaida zaidi kuliko wale wanaoyapanga au kuyahamasisha.
“Siasa za maendeleo zinapaswa kujengwa katika hoja na sera. Migogoro haijawahi kuleta suluhisho la kudumu,” amesema.
Pia alisisitiza umuhimu wa kuondoa kauli na vitendo vinavyoweza kuchochea mgawanyiko wa kijamii kwa misingi ya dini, kabila au maeneo ya kijiografia.
Katika maelezo yake kuhusu ziara za chama hicho, Kihongosi amesema CCM imebaini mwitikio mkubwa wa wananchi katika maeneo mbalimbali, ambapo wamekuwa wakieleza changamoto zao pamoja na kuridhishwa na miradi ya maendeleo.
Ameeleza ziara hizo zilizofanyika katika mikoa kadhaa na wilaya zaidi ya 40 zilitoa fursa ya kukutana moja kwa moja na wananchi na kusikiliza kero zao.
Kwa mujibu wake, wananchi wengi wameeleza kuona mabadiliko kupitia miradi ya maendeleo inayotekelezwa chini ya Serikali ya Awamu ya Sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan.
Ametaja maeneo kama afya, elimu, maji na barabara kuwa yameendelea kupokea uwekezaji mkubwa wa serikali.
Kihongosi amesema pia kuna maendeleo yanayoendelea kuonekana katika ukusanyaji wa mapato ya ndani, hali inayoiwezesha serikali kugharamia miradi mbalimbali ya maendeleo.
Akizungumzia nafasi ya CCM katika siasa za nchi, amesema chama hicho kinaendelea kuwa imara kutokana na mtandao wake mpana wa uongozi unaofika ngazi ya chini kabisa ya kijamii
Amesema hilo linaisaidia CCM kusikiliza na kushughulikia changamoto za wananchi kwa haraka zaidi.
Kuhusu hoja kwamba CCM ni chama cha wazee, ameeleza kuwa chama hicho kina wanachama wa makundi yote ya umri, na kwamba mchango wa wazee katika alisema ni muhimu na hauwezi kupuuzwa.


