Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
BAZECHA YAILILIA SERIKALI KUMWACHIA HURU TUNDU LISSU

BAZECHA YAILILIA SERIKALI KUMWACHIA HURU TUNDU LISSU


MatukioDaima Singida
‎Juni 25, 2026.
‎Wazee wa Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA) wameibuka na msimamo mpya wakitaka Serikali kumwachia huru Mwenyekiti wa chama hicho, Tundu Lissu, huku wakisisitiza kuwa kesi ya uhaini inayomkabili inapaswa kuendeshwa kwa haraka ili ipatiwe uamuzi. Kauli hiyo imetolewa katika mkutano wa siku mbili wa Baraza la Wazee wa CHADEMA (BAZECHA) uliofanyika mkoani Singida na kuhudhuriwa na wajumbe kutoka Tanzania Bara na Zanzibar.

‎Akizungumza baada ya mkutano huo, Mwenyekiti wa BAZECHA Taifa, Susan Lyimo, alisema azimio hilo ni moja ya maamuzi saba yaliyopitishwa na wajumbe kutoka kanda 10 za chama nchini. Alisema baraza hilo linaamini kuwa kumalizika kwa kesi hiyo kutasaidia kuondoa sintofahamu iliyodumu kwa muda mrefu.

‎Mbali na suala la Lissu, BAZECHA pia imekitaka chama kujaza haraka nafasi za uongozi zilizoachwa wazi kwa kufanya uchaguzi au uteuzi wa viongozi wa kukaimu. Pia kuanza mara moja kwa maandalizi ya maadhimisho ya miaka 20 ya mabadiliko ya Katiba ya CHADEMA ya mwaka 2006, yatakayofanyika Agosti 13 mwaka huu katika Kanda ya Pwani kupitia mkutano mkubwa wa hadhara.

‎Katika kuimarisha mshikamano wa wanachama, Lyimo alisema BAZECHA imeazimia kuunda kamati maalumu itakayosimamia programu za CHADEMA Family na BAZECHA Family, ambazo zitakuwa zikiratibu shughuli mbalimbali za kijamii ikiwemo misiba na sherehe kuanzia ngazi ya kata hadi taifa. Aidha, baraza hilo limeahidi kushiriki kikamilifu kampeni ya “Free Tundu Lissu” pamoja na programu nyingine za chama.

‎Washiriki wa mkutano huo, akiwemo Moses Balajaji na Naibu Katibu wa BAZECHA Taifa, Hamid Msaligundi, walisema mafunzo yaliyotolewa yatawasaidia wazee kukabiliana na changamoto za afya na maisha ya uzeeni, na wametoa wito kwa Watanzania kuendelea kuilinda demokrasia, kudumisha umoja na mshikamano wa kitaifa, kwa kuheshimu misingi ya utamaduni wa nchi.



 

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3