WIZARA YA VIWANDA NA BIASHARA YAOMBA BILIONI 137.8 KWA BAJETI YA MWAKA 2026/2027
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WIZARA ya Viwanda na Biashara imeiomba Bunge kuidhinisha bajeti ya Shilingi bilioni 137.8 kwa mwaka wa fedha 2026/2027 kwa ajili ya kutekeleza majukumu mbalimbali ya maendeleo ya sekta ya viwanda na biashara nchini.
Kati ya fedha hizo, Shilingi bilioni 104.1 zimetengwa kwa matumizi ya kawaida ya Wizara, ambapo Shilingi bilioni 78.0 zitatumika kwa ajili ya mishahara ya watumishi, huku Shilingi bilioni 26.0 zikitengwa kwa ajili ya matumizi mengineyo ya uendeshaji wa shughuli za kila siku za taasisi hiyo.
Akiwasilisha makadirio hayo ya bajeti Bungeni leo Mei 22, 2026 jijini Dodoma, Waziri wa Viwanda na Biashara, Judith Kapinga amesema Shilingi bilioni 33.6 zimetengwa mahsusi kwa ajili ya miradi ya maendeleo, ambapo fedha zote za maendeleo zimetokana na vyanzo vya ndani vya Serikali.
Amesema bajeti hiyo inalenga kuendelea kuimarisha mazingira wezeshi ya uwekezaji nchini, kuongeza uzalishaji wa viwanda vya ndani, kukuza biashara, pamoja na kuongeza ushindani wa bidhaa za Tanzania katika masoko ya ndani na ya kimataifa.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kimkakati kuhakikisha sekta ya viwanda inakua kwa kasi, ikiwemo kuboresha miundombinu ya uzalishaji, kurahisisha upatikanaji wa masoko kwa wazalishaji wa ndani, na kuhamasisha ushiriki wa sekta binafsi katika maendeleo ya uchumi wa viwanda.
Pia ameongeza kuwa utekelezaji wa bajeti hiyo utasaidia kuongeza ajira kwa wananchi, kuongeza mapato ya Serikali, na kuimarisha nafasi ya Tanzania katika ushindani wa kikanda na kimataifa kupitia bidhaa bora zinazozalishwa nchini.
