TAKUKURU YAZUIA VIONGOZI WA KIJIJI KUWATAPELI WAFUGAJI
May 22, 2026
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
TAASISI ya kuzuia na kupambana na rushwa (TAKUKURU) mkoa Kigoma imefanikisha kuokoa kiasi cha shilingi milioni 16 ambazo uongozi wa kijiji cha Mgambazi wilaya ya Uvinza mkoani Kigoma ulitaka kuwatapeli wafugaji wa kijiji hicho kwa madai ya kuingiza mifugo kwenye eneo la hifadhi ya msitu wa kijiji.
Naibu Mkuu wa TAKUKURU mkoa Kigoma, John Mgallah akitoa taarifa kwa waandishi wa habari mjini Kigoma alisema kuwa sambamba na kuokoa wafugaji hao kutapeliwa fedha hizo na uongozi wa kijiji pia wametoa maelekezo kwa uongozi wa serikali ya halmashauri ya wilaya Uvinza kuwachukulia hatua za kinidhamu viongozi na watendaji waliohusika na kadhia hiyo.
Akieleza kuhusu tukio hilo Mgallah alisema kuwa mfugaji aliyejulikana kwa jina la Paskali Donald na wenzake Machi mwaka huu walikamatwa wakiingiza jumla ya ng’ombe 204 kwenye hifadhi ya msitu wa kijiji hicho hivyo uongozi uliwakamata ng’ombe hao na kuamuru kila ng’ombe kulipiwa kiasi cha shilingi 80,000 sawa na jumla ya shilingi milioni 17 badala ya faini ya kisheria ya shilingi 5000 kwa kila ng’ombe sawa na shilingi milioni 1.2
Kwa mujibu wa taarifa hiyo uongozi wa kijiji cha Mgambazi ulitoa maelekezo kwa wafugaji hao kuwasilisha kwao pesa taslim na siyo kutumia mfumo wa malipo ya serikali jambo ambalo lilidhihirisha kuwa viongozi hao walikuwa na nia ovu ya kuwatapeli wafugaji hao.
Akizungumza na waandishi wa habari mmoja wa wafugaji hao, Paskali Donald alisema kuwa viongozi wa vijiji katika wilaya ya Uvinza wamekuwa na tabia ya kuwalipa faini kubwa ya ng;ombe zinazokamatwa kwa tuhuma ya kuingia kwenye hifadhi za msitu na hiyo imekuwa ikiwaingizia hasara kubwa kwao.
Mwisho.


