WIZARA YA ULINZI YAAINISHA MAENEO 8 YA KIPAUMBELE KWA MWAKA WA FEDHA 2026/2027...
May 20, 2026
Hamida Ramadhan Matukio Daima
Dodoma
Waziri wa Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa, Dkt. Rhimo Nyansaho, ametaja maeneo nane ya kipaumbele yatakayotekelezwa katika mwaka wa fedha 2026/2027 kwa lengo la kuimarisha sekta ya ulinzi nchini.
Akiwasilisha bajeti ya Wizara ya Ulinzi na Jeshi la Kujenga Taifa Bungeni jijini Dodoma leo Mei 19, 2026, Dkt. Nyansaho amesema Serikali itaendelea kuliimarisha jeshi kwa zana za kisasa, teknolojia, mawasiliano pamoja na rasilimali watu.
Amesema Serikali pia itaendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa wanajeshi, ikiwemo huduma za afya, makazi, mafunzo, mazoezi pamoja na maslahi yao.
Aidha, amesema Serikali itaendelea kuimarisha uwezo wa Jeshi la Kujenga Taifa kwa kuboresha miundombinu ili liweze kupokea vijana wengi zaidi kwa mafunzo ya kijeshi na stadi za kazi.
Katika hatua nyingine, amesema Serikali imepanga kuanzisha viwanda vipya vya sekta ya ulinzi vitakavyozalisha bidhaa za matumizi ya kijeshi na kiraia kwa kushirikiana na sekta binafsi.
Pia amesema Wizara itaendelea kuimarisha ushirikiano wa kimataifa katika masuala ya ulinzi pamoja na kushirikiana na mamlaka za kiraia kukabiliana na majanga na dharura mbalimbali nchini.

