WAZIRI MKUU ATAKA ELIMU ENDELEVU YA UHIFADHI WA ZIWA VICTORIA
NA CHAUSIKU SAID -MATUKIO DAIMA MWANZA.
MWANZA, WAZIRI Mkuu wa Jamhuri ya Muungano wa Tanzania, Dkt. Mwigulu Nchemba, amezitaka nchi wanachama wa Bonde la Ziwa Victoria kuweka mikakati endelevu ya kutoa elimu ya uhifadhi wa mazingira ya Ziwa Victoria kwa wananchi na wanafunzi ili kuhakikisha rasilimali hiyo muhimu inalindwa kwa manufaa ya kizazi cha sasa na kijacho.
Dkt. Nchemba amesema hayo leo Alhamisi Mei 21, 2026, wakati wa uzinduzi wa Siku ya Ziwa Victoria, hafla iliyoambatana na kuhitimishwa kwa maadhimisho yaliyoanza Mei 18 mwaka huu.
Dkt. Mwigulu Nchemba amesisitiza umuhimu wa utoaji wa elimu ya uhifadhi wa Ziwa Victoria kupitia shule na uanzishwaji wa klabu za mazingira ili kukuza utamaduni wa upandaji miti na utunzaji wa mazingira.
"ili kuhakikisha kunakuwa na uhifadhi endelevu wa Ziwa Victoria, ni muhimu kutoa elimu ya uhifadhi kwa wananchi, watoto na vijana kupitia shule za msingi na sekondari kwa kuanzisha klabu zinazojihusisha na masuala ya uhifadhi wa mazingira. Wekeni klabu zenye ushindani zitakazosaidia kujenga utamaduni endelevu wa upandaji miti na utunzaji wa mazingira," alisema Dkt. Mwigulu.
Kwa upande wake, Waziri wa Maji, Jumaa Aweso, amemshukuru Rais Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kuimarisha ushirikiano kati ya Tanzania na nchi wanachama wa Bonde la Ziwa Victoria, akisema hatua hiyo imesaidia kurahisisha utekelezaji wa shughuli mbalimbali za maendeleo katika ukanda huo.
Akizungumzia ripoti ya hali ya Bonde la Ziwa Victoria, Katibu Mtendaji wa Kamisheni ya Bonde la Ziwa Victoria, Bwire Masinde, amesema ziwa hilo linaendelea kukabiliwa na changamoto mbalimbali, ikiwemo suala la usalama wa usafiri majini, jambo linalohitaji ushirikiano wa pamoja katika kutafuta suluhisho la kudumu.
Naye Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda, amesema Ziwa Victoria limeendelea kuwa mhimili mkubwa wa uchumi wa Mkoa wa Mwanza kutokana na shughuli mbalimbali za kiuchumi zinazolitegemea.
Aidha, amesema ongezeko la vizimba vya samaki limechangia kuongeza ajira kwa vijana wengi mkoani humo na hivyo kuchochea maendeleo ya wananchi pamoja na uchumi wa eneo hilo.




