Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WASIRA: HATUPO TAYARI KUPOKEA AMRI ZA WAZUNGU

WASIRA: HATUPO TAYARI KUPOKEA AMRI ZA WAZUNGU

 



Na Fadhili Abdallah,Kigoma

 

 

Chama Cha Mapinduzi (CCM) kimesema kuwa serikali ya awamu ya sita inayoongozwa na Rais Samia Suluhu Hassan chini ya CCM   ipo tayari kupokea ushauri wa wadau mbalimbali kutoka popote duniani lakini haitatekeleza amri yeyote inayotolewa kutoka nje ya nchi katika utekelezaji wa majukumu ya serikali.


 

Makamu Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara, Stephen Wasira alisema hayo juzi jioni  akihutubia mkutano wa hadhara uliofanyika uwanja wa Kawawa Ujiji mjini Kigoma ikiwa ni sehemu ya ziara yake ya siku tatu mkoani Kigoma na kusema kuwa Tanzania ni nchii huru inayojiendesha na kuamua mambo yake bila kufuata amri au maelekezo ya mtu yeyote.



 

Alisema kuwa watu wana midomo na ni haki yao kusema na wengine wameweka mawakala nje ya nchi kwa ajili ya kuwasemea hivyo wanawapa nafasi ya kusema  lakini serikali ya Tanzania haitafuata amri au maelekezo wanayotoa  ikiwemo kutaka uchaguzi ufanyike upya kwa sababu uliofanyika Oktoba 29 mwaka jana haukuwa wa kidemokrasia.



Kutokana na hilo Makamu huyo Mwenyekiti wa CCM Tanzania Bara aliwataka  vijana ambao ni asilimia 65 ya Watanzania  kutokubali kutumika kuvuruga nchi yao kwa maslahi ya  watu wa nje wasioitakia mema Tanzania na badala yake washikamane kuijenga na kuleta maendeleo ya nchi yao.

 



Wasira alisema kuwa hakuna mtu anayependa  vifo vitokee lakini yaliyotokea Oktoba 29 yanajulikana hivyo ametaka waliofanya hayo wajulikane, sheria ichukue mkondo wake mwisho nchi iende kwenye maridhiano na kuwa  kitu kimoja katika kujenga nchi na kutekeleza mipango ya maendeleo.


“Wazungu wanaotoa amri ya kutaka tufanye wanachotaka waliondoka na kutuacha tukiwa hatuna kitu tumetumia muda na rasilimali nyingi kuijenga nchi yetu kwa ajili ya Watanzania, watuachie tuijenge nchi yetu, tuko tayari kupokea ushauri kutoka popote duniani bila ubaguzi lakini  hatuko tayari kupokea amri, maana hiyo ni kubeba uhuru wetu,”Alisema Stephen Wasira.





Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3