Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
UWAMAKIZI YAONGOZA MAPAMBANO DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI BONDE LA ZIGI

UWAMAKIZI YAONGOZA MAPAMBANO DHIDI YA MABADILIKO YA TABIANCHI BONDE LA ZIGI

Na Amina Saidi,  

Matukio Daima Media,Tanga.

KATIKA mwaka huu wa fedha 2025/2026, Umoja wa Wakulima Wahifadhi Mazingira Kihuhwi–Zigi (UWAMAKIZI) kwa kushirikiana na Tanga UWASA umeendelea kutekeleza shughuli za uhifadhi wa mazingira na usimamizi wa vyanzo vya maji katika bonde la Zigi, ikiwa ni sehemu ya mikakati ya kukabiliana na athari za mabadiliko ya tabianchi.


Shughuli hizo zinatekelezwa kupitia miradi mbalimbali ikiwemo Land and Sustainable Agriculture (LSA) inayofadhiliwa na GIZ chini ya mpango wa Green and Smart City SASA pamoja na programu ya Ecosystem-based Payment for Water Services (EPWS), ambazo zimekuwa chachu ya kuimarisha ushirikiano wa jamii na taasisi katika uhifadhi wa mazingira.


Katika utekelezaji wa programu hizo, zaidi ya wakulima 1,012 kutoka vijiji 14 vipya wamepatiwa elimu ya kilimo hifadhi na kilimo mseto, pamoja na kushiriki katika mikutano ya uhamasishaji kuhusu utunzaji wa vyanzo vya maji, hatua inayolenga kupunguza athari za ukame na mmomonyoko wa ardhi.


Aidha, jumla ya miche 165,200 imeandaliwa katika vitalu mbalimbali vya miti ya biashara na asili, huku juhudi za kuanzisha vitalu vipya na vikundi vya wakulima zikiongezeka, ikiwa ni mkakati wa kuongeza uoto wa asili na kuhakikisha upatikanaji endelevu wa miche kwa shughuli za upandaji miti.


Katika hatua nyingine, zaidi ya miti 95,035 imepandwa katika maeneo mbalimbali ya bonde la Zigi, ambapo kilomita 33.6 za kingo za mito zimeimarishwa kupitia upandaji huo.

 Hatua hii imeelezwa kuwa muhimu katika kupunguza mmomonyoko wa udongo, kulinda vyanzo vya maji na kuongeza ustahimilivu wa mazingira dhidi ya mabadiliko ya tabianchi.

Hata hivyo, taarifa zinaonesha kuwa ukame mkali uliosababishwa na kukosekana kwa mvua za vuli umeathiri kiwango cha maji katika mito na vijito, hali inayoendelea kuathiri shughuli za kilimo na maisha ya wananchi, hivyo kuhitaji hatua za haraka na endelevu za kukabiliana na changamoto za tabianchi.


Akizungumzia mafanikio hayo, Hassan Singano ambaye ni Makamo Mwenyekiti wa   UWAMAKIZI amesema wamejidhatiti  kuhakikisha jamii inakuwa mstari wa mbele katika kulinda mazingira.

 “Kupitia elimu ya kilimo hifadhi na upandaji miti, jamii imeanza kuona mabadiliko chanya katika kurejesha uoto na kulinda vyanzo vya maji,” alisema Singano.

Kwa upande wake, Ramadhan Nyambuka ambaye ni Mratibu wa Mazingira Tanga Uwasa alisisitiza umuhimu wa ushirikiano wa wadau katika kukabiliana na mabadiliko ya tabianchi, akieleza kuwa juhudi za pamoja ndizo zitakazohakikisha uendelevu wa rasilimali za maji.

 “Ulinzi wa vyanzo vya maji si jukumu la taasisi moja, bali ni la jamii nzima na wadau wote,” aliongeza Nyambuka.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3