AREPTA YATAKA SHERIA KALI KUDHIBITI MADALALI WA ARDHI
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WAKATI Serikali ikiendelea na mchakato wa kuimarisha usimamizi wa sekta ya milki nchini, wadau wameeleza wasiwasi wao kuhusu kuendelea kuwepo kwa madalali wa ardhi wanaofanya kazi bila usajili huku hata waliosajiliwa wakitakiwa kufanya kazi chini ya wataalamu wa sekta hiyo ili kulinda wananchi dhidi ya utapeli na hasara.
Akizungumza katika Mkutano Mkuu wa Mwaka na Kongamano la AREPTA, Rais wa chama hicho, Boniphace Yumba, amesema hali hiyo imekuwa ikichangia kuharibika kwa taswira ya sekta ya ardhi pamoja na kuongeza migogoro na malalamiko kutoka kwa wananchi.
Yumba amesema bado kuna changamoto ya uwepo wa madalali wasiokuwa na usajili ambao wamekuwa wakifanya shughuli za milki bila kufuata utaratibu wa kitaaluma.
Amesema hata wale waliosajiliwa wanapaswa kufanya kazi chini ya usimamizi wa wataalamu wa sekta hiyo ili kuongeza uwajibikaji na ulinzi kwa wananchi.
“Sheria ya udhibiti wa milki itasaidia shughuli zote zinazohusiana na milki kusimamiwa kitaalamu na kwa mujibu wa sheria. Bila sheria hiyo, hatari nyingi zitaendelea kuwepo na wananchi wataendelea kupata athari katika sekta hii muhimu ambayo ni uti wa mgongo wa maendeleo ya taifa,” amesema Yumba.
Kwa upande wake, Katibu wa chama hicho, Linda Msaki, amesema mkutano huo unatarajiwa kutoka na maadhimio yatakayosaidia kufanikisha ndoto ya muda mrefu ya kuanzishwa kwa mamlaka ya kusimamia sekta ya milki nchini (Real Estate Regulatory Authority).
Msaki amesema ajenda hiyo ni miongoni mwa mambo makuu yanayojadiliwa katika kongamano hilo sambamba na mikakati ya utekelezaji wa mfumo wa uchangiaji wa pamoja katika uwekezaji wa milki, jambo ambalo linaelezwa kuwa na mchango mkubwa katika kukuza uchumi wa taifa.
Naye Kamishna wa Ardhi, Nathaniel Nonge, aliyemwakilisha Waziri wa Ardhi, Nyumba na Maendeleo ya Makazi, amesema Serikali inatambua changamoto zilizowasilishwa na wadau wa sekta hiyo na ipo tayari kushirikiana nao katika kuhakikisha mfumo wa usimamizi wa sekta ya milki unaimarishwa.
Amesema hatua za kuanzisha chombo cha usimamizi wa sekta hiyo zinaendelea vizuri na Serikali inalifanyia kazi suala hilo kwa karibu ili kuhakikisha sekta ya milki inakuwa na usimamizi wenye tija unaolinda maslahi ya wananchi na wawekezaji.
Mwisho



