Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
UCSAF YAONGEZA KASI YA UPATIKANAJI WA INTANETI BURE NCHINI

UCSAF YAONGEZA KASI YA UPATIKANAJI WA INTANETI BURE NCHINI

 


Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma

MFUKO wa Mawasikiano kwa Wote (UCSAF) umeendelea kuimarisha jitihada za Serikali katika kupanua upatikanaji wa huduma za intaneti bure kwa wananchi kupitia utekelezaji wa mradi wa huduma za intaneti katika maeneo ya wazi yenye matumizi makubwa ya wananchi.

Akizungumza kwenye mafunzo ya wahariri na waandishi wa habari jijini Dodoma kuhusu utekelezaji wa mradi huo, Kaimu Mtendaji Mkuu wa UCSAF, Mhandisi Albert Richard, amesema lengo la mradi huo ni kuongeza upatikanaji wa huduma za mawasiliano, kukuza matumizi ya TEHAMA na kuwezesha wananchi kushiriki kikamilifu katika uchumi wa kidijitali.

“Mfuko unaendelea kuhakikisha wananchi wanapata huduma za intaneti katika maeneo muhimu ya kijamii na kiuchumi ili kuongeza fursa za elimu, biashara na upatikanaji wa taarifa kwa urahisi zaidi,” amesema Mhandisi Richard.

Kupitia mradi huo, vituo 17 vya huduma ya intaneti bure vimeanzishwa katika Viwanja vya Maonesho ya Kimataifa ya Biashara ya Sabasaba.


 Aidha, huduma hizo zimefikishwa katika maeneo mbalimbali nchini ikiwemo Nyerere Square, College of Informatics CIVE, Soko la Nyamagana, Kiembesamaki, Soko la Tabora pamoja na Lungemba Training College.


Katika mwaka wa fedha 2024/2025, UCSAF ilitekeleza mradi huo katika maeneo 25 ya vituo vya mabasi ya mwendokasi vya DART kwa gharama ya jumla ya shilingi milioni 500.


Aidha, kwa mwaka wa fedha 2025/2026, utekelezaji wa mradi huo unaendelea katika maeneo 60 ya Tanzania Bara na Zanzibar, hatua inayotarajiwa kuongeza upatikanaji wa huduma za intaneti kwa wananchi wengi zaidi pamoja na kuchochea maendeleo ya uchumi wa kidijitali nchini.


Wadau wa sekta ya mawasiliano wameeleza kuwa utekelezaji wa miradi hiyo utaongeza matumizi ya teknolojia, kuimarisha utoaji wa huduma za kidijitali na kufungua fursa mpya za maendeleo kwa jamii.


Awali akifungua mafunzo hayo, Afisa Mawasiliano Mwandamizi wa UCSAF, Celina Mwakabwale amesema kuwa uelewa mdogo wa masuala ya kitaalam sambamba na ongezeko la taarifa za uchochezi na upotoshaji bado ni miongoni mwa changamoto kubwa zinazokwamisha utoaji wa habari sahihi kwa umma.


Celina amesema changamoto hiyo imeendelea kujitokeza katika baadhi ya vyombo vya habari na majukwaa ya mitandao ya kijamii, ambapo taarifa husambazwa bila kufanyiwa uchambuzi wa kina na uhakiki wa kutosha, hali inayoweza kupotosha jamii na kuathiri uelewa wa wananchi kuhusu masuala muhimu.

“Ni muhimu kwa waandishi wa habari kujijengea uwezo na maarifa ya kutosha katika masuala ya kitaalam ili kuepusha upotoshaji wa taarifa ambao unaweza kusababisha taharuki, migogoro na kuvuruga mshikamano wa jamii,” amesema Celina.

Aidha, ameonya dhidi ya ongezeko la matumizi ya lugha za uchochezi katika utoaji wa habari, akieleza kuwa vyombo vya habari vina wajibu mkubwa wa kulinda amani, utulivu na mshikamano wa taifa kwa kuhakikisha taarifa zinazorushwa au kuchapishwa zinazingatia ukweli, weledi na maadili ya taaluma ya habari.


Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3