TAKUKURU YASAIDIA KUREJESHA SHILINGI MILIONI 167, SINGIDA
Na Matukio Daima Media ,Singida.
Mapato ya halmashauri za wilaya za Iramba na Manyoni mkoani Singida, zaidi ya Sh milioni 56.4 zilizokuwa katika hatari ya kupotea kupitia makusanyo ya ushuru, zimerejeshwa serikalini baada ya Taasisi ya Kuzuia na Kupambana na Rushwa (TAKUKURU), kufanya ufuatiliaji wa kina wa matumizi ya mashine za kielektroniki za ukusanyaji mapato (POS).
Fedha hizo ni sehemu ya Sh 167,725,810 zilizookolewa na kurejeshwa serikalini kupitia uchunguzi wa matumizi ya fedha za miradi ya maendeleo, mashitaka ya ubadhirifu wa mali za umma pamoja na upotevu wa mapato katika mifumo ya ukusanyaji ushuru mkoani Singida.
Akizungumza na waandishi wa habari kuhusu utekelezaji wa majukumu ya TAKUKURU kwa kipindi cha Januari hadi Machi 2026, Mkuu wa TAKUKURU Mkoa wa Singida, Sosthenes Kibwengo amesema mafanikio hayo yametokana na ushirikiano mkubwa wa wananchi pamoja na wadau mbalimbali wanaoshiriki katika mapambano dhidi ya rushwa.
Kibwengo amesema pamoja na fedha hizo kurejeshwa serikalini, uchunguzi bado unaendelea katika baadhi ya maeneo ili kubaini wahusika na kuchukua hatua za kisheria kulingana na taratibu zilizopo.
Ameeleza kuwa katika ufuatiliaji wa matumizi ya fedha za utekelezaji wa miradi ya maendeleo, TAKUKURU ilichunguza miradi 28 yenye thamani ya Sh 8,231,350,232 inayohusisha sekta za elimu, afya, barabara, maji na utawala, na kufanikiwa kurejesha Sh 76,729,768 serikalini.
Kwa mujibu wa Kibwengo, fedha hizo zilirejeshwa baada ya kubainika kuwepo kwa wazabuni walioshindwa kupeleka vifaa vya ujenzi kwenye maeneo ya miradi, vifaa visivyokuwa na ubora unaotakiwa pamoja na masurufu yaliyotumika kinyume cha utaratibu katika mradi wa ujenzi wa madarasa wa Shule ya Sekondari Kintinku wilayani Manyoni.
Ametaja maeneo mengine yaliyobainika kuwa na upotevu wa fedha kuwa ni kodi ya ongezeko la thamani (VAT) pamoja na kodi za zuio zilizokatwa kwa wazabuni wa vifaa vya ujenzi lakini kutowasilishwa Mamlaka ya Mapato Tanzania (TRA) kama sheria inavyotaka.
Akizungumzia uchunguzi wa mashitaka, Kibwengo amesema TAKUKURU imefanikiwa kurejesha Sh 34,448,042 zilizotokana na uchunguzi wa kesi za ubadhirifu wa mali za umma, huku taasisi hiyo ikipokea malalamiko 95 katika kipindi hicho, ambapo 51 yalihusiana moja kwa moja na vitendo vya rushwa.
Katika hatua nyingine, amesema TAKUKURU imeendelea kutoa elimu kwa umma kwa kuwafikia wananchi 79,465 kupitia mikutano 76, kuimarisha klabu 106 za kupinga rushwa na kutoa elimu kwa makundi 40 kati ya 50 yanayotambuliwa na taasisi hiyo mkoani Singida.
MWISHO

