PEEC YAKABIDHI MICHE 100 YA MIKOROSHO KWA PANGAWE SEKONDARI
Na Matukio Daima, Morogoro
Shirika la People Education and Environmental Conservation (PEEC), Dkt. Saida Fundi, amekabidhi miche 100 ya mikorosho kwa Shule ya Sekondari Pangawe mkoani Morogoro kwa lengo la kuhamasisha upandaji wa miti ya kibiashara na kuimarisha uhifadhi wa mazingira.
Mwenyekiti wa PEEC Dkt. Saida amesema miche hiyo itasaidia kuongeza uoto wa asili, kupunguza athari za mabadiliko ya tabianchi na kuwa chanzo cha mapato kwa shule kupitia mauzo ya korosho katika siku zijazo.
Amesema PEEC itaendelea kushirikiana na taasisi za elimu katika kukuza utamaduni wa upandaji miti yenye manufaa ya kiuchumi na kimazingira.
Mkuu wa shule hiyo Dorice Luhanga pamoja na Dada Mkuu Rehema Athman wameshukuru shirika la PEEC kwa msaada huo, huku wanafunzi wakiahidi kuitunza miche hiyo ili iweze kukua na kuleta manufaa kwa shule na jamii inayozunguka.





