PAMS FOUNDATION YAKABIDHI HATI MILKI, GESI ,MADAWATI NA KUZINDUA UPANDAJI MITI MVOMERO
Na Matukio Daima, Mvomero
TAASISI ya Pams (Pams Foundation) kupitia mradi wake wa urejeshaji wa uoto wa asili katika Milima ya Nguru imekabidhi hati milki za kimila 293, mitungi ya gesi 25, madawati 30 na mabenchi 30 kati ya 40 kwa wananchi wa vijiji vya Pemba na Gonja wilayani Mvomero mkoani Morogoro sambamba na uzinduzi wa zoezi la upandaji miti.
Akizungumza wakati wa hafla hiyo, Mratibu wa mradi huo, Richard John, amesema hatua hiyo inalenga kusaidia utunzaji wa mazingira kwa kupunguza matumizi ya nishati chafu pamoja na kuwawezesha wananchi kushiriki katika shughuli za maendeleo kupitia matumizi bora ya ardhi na biashara ya hewa ukaa.
Amesema wananchi wa vijiji vya Pemba na Gonja wamekabidhiwa hati milki za kimila huku wananchi wengine wakipatiwa mitungi ya gesi yenye majiko yake ili kuhamasisha matumizi ya nishati safi na kupunguza ukataji miti ovyo.
Mkuu wa wilaya ya Mvomero akimkabidhi mwalimu mkuu wa shule ya msingi pemba moja ya dawati kama ishara ya kukabidhi madawati 30 yaliyotolewa
Kwa upande wake, Maximilian Genes, msimamizi wa miradi kutoka Pams Foundation, amesema mradi huo umeendelea kusaidia kurejesha uoto wa asili katika ukanda wa Milima ya Nguru huku wananchi wakinufaika kupitia ajira, elimu ya kilimo bora na umilikishaji wa ardhi.
Akasema Nia ya kutoa hati milki ni ili kuwahakikishia Wananchi umiliki wa maeneo Yao na kwamba mradi unachofanya ni kuwahamasisha watumie kupanda miti kukabiliana na mabadiliko ya tabia nchi na baadaye kuuza hewa ya ukaa.
Akizungumza katika uzinduzi huo,Mkuu wa wilaya ya Mvomero, Maulid Dotto, amewataka wananchi kushiriki kikamilifu katika kulinda misitu na mazingira huku akionya dhidi ya vitendo vya uvamizi wa maeneo ya hifadhi, uchomaji moto ovyo na uvunaji haramu wa mazao ya misitu.
Amesema wilaya hiyo inaendelea kukabiliwa na changamoto za uharibifu wa mazingira katika baadhi ya maeneo ya hifadhi ikiwemo Msitu wa Mkingu kutokana na shughuli za kibinadamu.
Naye Mkurugenzi Mtendaji wa halmashauri ya wilaya ya Mvomero, Paulo Phaty, amesema matumizi bora ya ardhi pamoja na matumizi ya nishati safi ni muhimu katika kuhifadhi mazingira na kuboresha maisha ya wananchi.
Baadhi ya wananchi walionufaika na mradi huo akiwemo Omary Kivumbi wa Kijiji cha Pemba amesema licha ya umri wake kuwa mkubwa, kupitia mradi huo ameweza kupata hati milki pamoja na elimu ya kilimo bora cha viazi iliyomsaidia kuongeza uzalishaji wa mazao na kipato chake sambamba Kilimo cha miti.
Naye Fitina Athumani wa Kijiji cha Gonja amesema kupatiwa jiko la gesi kutamsaidia kuachana na matumizi ya kuni na mkaa ambayo yamekuwa yakichangia uharibifu wa mazingira huku akiahidi kuwa balozi wa matumizi ya nishati safi katika kijiji chake.
Aidha Selemani Madaraka wa Kijiji cha Gonja amesema hati milki walizopata zitawasaidia kulinda maeneo yao dhidi ya uvamizi pamoja na kuwapa fursa ya kupata mikopo kwa ajili ya shughuli za maendeleo na kwamba hii ni mara ya kwanza kwake kuanza kutumia nishati ya gesi kupikia.




