MWENGE WA UHURU KUZINDUA MIRADI 39 MKOANI IRINGA
Na Easter Kameta – Matukio Daima Media
Mkuu wa Mkoa wa Iringa, Kheri James, amewataka wananchi wa mkoa huo kujitokeza kwa wingi kushiriki mapokezi ya Mwenge wa Uhuru utakaowasili mkoani Iringa tarehe 26 Mei 2026 katika viwanja vya Shule ya Sekondari Marangali, wilayani Mufindi.
Akizungumza na Matukio Daima, Kheri amesema Mwenge wa Uhuru utapokelewa kutoka mkoa wa Njombe na utatembelea wilaya zote tano za Mkoa wa Iringa kwa umbali wa kilomita 623.8.
Katika mbio hizo, jumla ya miradi 39 itazinduliwa, kukaguliwa, kutembelewa pamoja na kuwekewa mawe ya msingi. Miradi hiyo ina thamani ya zaidi ya shilingi bilioni 107.5.
“Kila mwananchi anapaswa kushiriki katika shughuli hizi muhimu za maendeleo,” amesema Kheri.
Aidha, amesema kaulimbiu ya Mwenge wa Uhuru mwaka huu ni: “Tanzania ni yetu, sote tuungane na kushikamana kuleta maendeleo.”
Mkuu huyo wa mkoa ametoa rai kwa watumishi wa umma, viongozi na wadau mbalimbali wa maendeleo kushiriki kikamilifu katika mapokezi na shughuli zote za Mwenge wa Uhuru katika halmashauri zote za Mkoa wa Iringa kulingana na ratiba zilizopangwa.
Amesema ujio wa Mwenge wa Uhuru ni fursa muhimu kwa wananchi kupata taarifa kuhusu utekelezaji wa miradi ya maendeleo katika maeneo yao, kufahamu hatua zilizofikiwa, pamoja na kuimarisha umoja, mshikamano na shughuli za kiuchumi.
“Mwenge wa Uhuru pia utachochea shughuli za biashara kutokana na wananchi kupeleka bidhaa zao katika maeneo mbalimbali yatakayopitiwa na mwenge, hali itakayoongeza mzunguko wa fedha,” amesema.
Vilevile, amewapongeza vijana waliochaguliwa kushiriki katika mbio za Mwenge wa Uhuru ngazi ya mkoa na wilaya kwa kuaminiwa kuwa na nidhamu, weledi na uwezo wa kuhakikisha shughuli hiyo inafanikiwa kuanzia mwanzo hadi mwisho.
Kwa mujibu wa Kheri, timu hiyo pia itasaidia katika utoaji wa huduma za afya endapo kutatokea changamoto, pamoja na kusaidia masuala ya kiitifaki, uratibu na usimamizi wa shughuli zote zinazohusiana na mbio za Mwenge wa Uhuru.

