MTANDA ATOA RAI KWA WANANCHI KUSHIRIKIANA NA POLISI KUPAMBANA NA UHALIFU.
NA CHAUSIKU SAID
MATUKIO DAIMA MWANZA.
MWANZA, Mkuu wa Mkoa wa Mwanza, Said Mtanda. amewataka wananchi kuendelea kushirikiana na Jeshi la Polisi kupitia Kamisheni ya Polisi Jamii ili kuimarisha mapambano dhidi ya vitendo vya uhalifu.
Mtanda alisema hayo Mei 9 katika maadhimisho ya Siku ya Familia ya Jeshi la Polisi yaliyofanyika katika uwanja wa Nyamagana Wilaya ya Nyamagana Mkoani hapa na kueleza kuwa ushirikiano kati ya polisi na wananchi ni nguzo muhimu katika kudhibiti uhalifu na kutoa taarifa za wahalifu kwa wakati.
“Tunapaswa kuendelea kuimarisha Polisi Jamii ili iwe kiungo kizuri kati ya wananchi na Jeshi la Polisi. Ushirikiano huu utasaidia kuzuia na kudhibiti vitendo vya uhalifu katika maeneo yetu,” amesema Mtanda.
Aidha hata hivyo Mtanda, amelipongeza Jeshi la Polisi Mkoa wa Mwanza kwa kazi kubwa wanayoendelea kuifanya katika kuhakikisha amani, utulivu na usalama vinaendelea kudumu ndani ya mkoa huo.
Amesema kuwa kazi inayofanywa na askari wa jeshi hilo imekuwa chachu ya maendeleo kutokana na wananchi kuendelea kufanya shughuli zao za kiuchumi katika mazingira salama na yenye utulivu.
Amesema serikali inatambua mchango mkubwa wa Jeshi la Polisi katika kulinda raia na mali zao, huku akiwasisitiza askari kuendelea kufanya kazi kwa bidii, uadilifu na uzalendo mkubwa kwa taifa.
“Jeshi la Polisi limeendelea kufanya kazi nzuri ya kuimarisha ulinzi na usalama. Serikali inatambua na kuthamini juhudi zinazofanywa na askari wetu katika kuhakikisha wananchi wanaishi kwa amani na usalama wakati wote,” amesema Mtanda.
Amesema serikali ya awamu ya sita imeendelea kuboresha mazingira ya kazi kwa askari polisi nchini kupitia utekelezaji wa miradi mbalimbali ikiwemo ujenzi wa vituo vya polisi, nyumba za askari pamoja na kuongeza vitendea kazi vya kisasa.
Ameeleza kuwa hatua hizo zina lengo la kuongeza ufanisi wa utendaji kazi ndani ya Jeshi la Polisi na kuwawezesha askari kutekeleza majukumu yao kwa weledi na uharaka zaidi.
“Serikali imeendelea kupandisha vyeo askari, kujenga vituo vya polisi na nyumba za askari pamoja na kuongeza vitendea kazi kama magari na vifaa mbalimbali vya kiutendaji ili kuhakikisha jeshi linafanya kazi katika mazingira bora,” ameongeza.
Kwa hatua nyingine Mtanda amegusia changamoto ya uhalifu wa mitandao na kueleza kuwa kuna umuhimu mkubwa wa kuimarisha mifumo ya uchunguzi wa kisasa ili kukabiliana na wahalifu wanaotumia teknolojia kufanya uhalifu.
Amesema maendeleo ya teknolojia yameleta manufaa makubwa lakini pia yameongeza aina mpya za uhalifu, hivyo kuna haja ya vyombo vya usalama kwenda sambamba na mabadiliko hayo ya kidijitali.
Mtanda amesema serikali inaendelea kuchukua hatua mbalimbali za kuimarisha uwezo wa askari katika matumizi ya mifumo ya kidijitali ili kusaidia uchunguzi wa makosa ya jinai na kudhibiti uhalifu wa mitandao.
Kwa upande wake, Kamanda wa Polisi Mkoa wa Mwanza (RPC), Wilbroad Mutafungwa, amesema mkoa wa Mwanza unaendelea kuwa katika hali ya utulivu kutokana na ushirikiano mzuri uliopo kati ya Jeshi la Polisi, wananchi pamoja na vyombo mbalimbali vya ulinzi na usalama.
Amesema Jeshi la Polisi linaendelea kutekeleza majukumu yake kwa kuzingatia misingi ya taaluma, uwajibikaji na haki ili kuhakikisha wananchi wanapata huduma bora za
kiusalama.
Amesema Jeshi la Polisi litaendelea kushirikiana na jamii katika kutatua changamoto mbalimbali za kiusalama ili kuhakikisha wananchi wanaendelea kuishi kwa amani na kufanya shughuli zao za maendeleo bila hofu.
Maadhimisho hayo ya Siku ya Familia ya Jeshi la Polisi yamelenga kuimarisha mshikamano kati ya askari polisi, familia zao pamoja na wananchi, sambamba na kutambua mchango wa jeshi hilo katika kudumisha amani na usalama nchini.







