MBEYA CITY EXPO 2026 KUFUNGUA MILANGO YA BIASHARA NA UWEKEZAJI KANDA YA NYANDA ZA JUU KUSINI
Na Samwel Mpogole Mbeya.
Mkuu wa Mkoa wa Mbeya Beno Malisa, kwa kushirikiana na Chemba ya Taifa ya Biashara Tanzania (TNCC) Mkoa wa Mbeya, amewataka wananchi, wafanyabiashara na wawekezaji kujitokeza kwa wingi kushiriki maonesho ya Mbeya City Expo 2026 msimu wa nne yatakayofanyika kuanzia Mei 22 hadi 30 katika viwanja vya Uhindini Jijini Mbeya.
Akizungumza na waandishi wa habari, Mkuu wa Mkoa amesema maonesho hayo yenye kaulimbiu ya “Kujenga Uchumi wa Kikanda kupitia Biashara na Uwekezaji” yanalenga kukuza biashara, uwekezaji pamoja na kuwakutanisha wafanyabiashara kutoka ndani na nje ya nchi ikiwemo Malawi, Zambia na Zimbabwe.
Amesema wananchi watapata nafasi ya kujifunza fursa mbalimbali za biashara na uwekezaji pamoja na kupata huduma kutoka taasisi tofauti zikiwemo Taasisi ya Mifupa MOI na Hospitali ya Rufaa Kanda ya Mbeya.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa TNCC Mkoa wa Mbeya, Erick Sichinga amesema maandalizi ya maonesho hayo yamekamilika huku akiwakaribisha wafanyabiashara, taasisi na wananchi kushiriki ili kutumia fursa ya kutangaza bidhaa na huduma zao pamoja na kujenga mtandao wa biashara.
Maonesho hayo yanatarajiwa kufunguliwa rasmi na Waziri wa Nchi Ofisi ya Rais Mipango na Uwekezaji, Profesa Kitila Mkumbo (MB) na kufungwa na Waziri wa Viwanda na Uwekezaji, Judith Kapinga(MB).
.jpeg)
