KIJANA MZALENDO BLACK ATOA ZAWADI YA MAFUTA KWA BODABODA IRINGA AKIHIMIZA UZALENDO
Kijana mzalendo Alphonce Myinga, maarufu kwa jina la Black, ameendelea kujipambanua kama mhamasishaji wa uzalendo kwa vitendo baada ya kutoa msaada wa mafuta kwa zaidi ya vijana 100 wa bodaboda katika mji wa Iringa.
Hatua hiyo imekuja ikiwa ni sehemu ya maadhimisho ya Sikukuu ya Wafanyakazi, akilenga kuhamasisha vijana kuipenda nchi yao na kushiriki kikamilifu katika kulinda amani ya taifa.
Akizungumza na waandishi wa habari mara baada ya kukabidhi msaada huo, Black alisema kuwa amekuwa akifanya juhudi mbalimbali kupitia mitandao ya kijamii kuelimisha vijana kuhusu umuhimu wa uzalendo. Alieleza kuwa kupitia juhudi hizo, alipokea mchango wa shilingi milioni moja kutoka kwa mdau mmoja anayependa amani, ambaye aliguswa na kazi yake ya kuhamasisha jamii.
Black alifafanua kuwa baada ya kupokea fedha hizo, aliamua kuzitumia kwa namna itakayokuwa na manufaa ya moja kwa moja kwa vijana wenzake, hasa wale wa bodaboda ambao ni sehemu muhimu ya jamii. Alisema kuwa kundi hilo lina nafasi kubwa ya kuwa mabalozi wa amani kutokana na kukutana na watu wa rika na mitazamo mbalimbali kila siku katika shughuli zao za usafirishaji.
“Niliona ni vyema kurejesha fedha hizi kwa jamii kwa kuwasaidia vijana wa bodaboda. Lengo langu ni kuwahamasisha sio tu kufanya kazi kwa bidii, bali pia kuwa mstari wa mbele katika kueneza ujumbe wa amani na uzalendo,” alisema Black.
Aidha, alieleza kuwa kuchagua kuanza zoezi hilo mkoani Iringa ni kutokana na ukweli kuwa ni nyumbani kwake, lakini mpango wake ni kuendelea na kampeni hiyo katika maeneo mengine nchini. Alisisitiza kuwa dhamira yake ni kufikia vijana wengi zaidi na kuwahamasisha kuwa sehemu ya kulinda tunu za taifa.
Katika nasaha zake kwa vijana, Black aliwataka kuwa makini na kuepuka kushawishiwa na watu au makundi yenye nia ya kuvuruga amani ya nchi.
Alionya kuwa kuna baadhi ya watu, iwe ni wa ndani au nje ya nchi, wanaoweza kujaribu kupandikiza chuki au vurugu, jambo ambalo linaweza kuhatarisha usalama na ustawi wa taifa.
Alisisitiza kuwa Tanzania ni nchi moja yenye umoja na mshikamano, na kwamba hakuna mbadala wa amani iliyopo. “Tanzania ni moja, na hatuna nchi nyingine ya kukimbilia. Tukichezea amani yetu, madhara yake yatakuwa makubwa kwa kila mmoja wetu,” aliongeza.
Black pia aliwahimiza vijana kuendelea kuunga mkono juhudi za serikali katika kuleta maendeleo, akieleza kuwa maendeleo hayawezi kupatikana bila kuwepo kwa amani.
Alitaja juhudi zinazofanywa na Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kuwa ni mfano wa dhamira ya dhati ya kuijenga nchi, hivyo zinahitaji ushirikiano wa wananchi wote, hasa vijana.
Alisema kuwa vijana wa bodaboda wana jukumu kubwa katika jamii, hivyo wanapaswa kutumia nafasi yao kuhamasisha mshikamano na kuishi kwa amani.
Hata hivyo alisema kuwa ataendelea kushirikiana na wadau mbalimbali katika kuendeleza maadili mema na uzalendo kwa Taifa.
Kwa upande wake, Mwenyekiti wa bodaboda mkoani Iringa, Zuberi Mapilla, alimpongeza Black kwa msaada huo, akisema umeleta faraja kubwa kwa vijana wa bodaboda.
Kuwa msaada huo utawasaidia kupunguza changamoto wanazokutana nazo katika kazi zao za kila siku hasa ukizingatia bei kubwa ya mafuta sasa.
Mapilla alisema kuwa pamoja na msaada huo, ujumbe uliotolewa wa kuhimiza amani ni muhimu zaidi kwa vijana wa bodaboda.
Aliwataka boda boda na vijana wengine nchini kuendelea kuwa walinzi wa amani na kuepuka vitendo vyovyote vinavyoweza kuhatarisha utulivu wa nchi.
"msaada huu Black umeonyesha kuwa uzalendo unaweza kuonyeshwa kwa vitendo vinavyogusa maisha ya watu moja kwa moja kuwa msaada huo umeacha alama ya matumaini na kuhamasisha vijana wengi zaidi kushiriki katika kujenga taifa lenye amani, umoja na maendeleo endelevu"




