Kwa Habari za kitaifa, Kimataifa, Michezo, Burudani,Uchambuzi na matangazo. Matukio Daima Blog, Ni yetu Sote!
WAKAZI WA MTAMA KUACHA SAFARI YA KM 7 KUFUATA HUDUMA YA X-REY NYANGAO

WAKAZI WA MTAMA KUACHA SAFARI YA KM 7 KUFUATA HUDUMA YA X-REY NYANGAO


Na Hadija Omary Lindi..

Kwa miaka mingi wananchi wanaopata huduma katika Kituo cha Afya Mtama wamelazimika kusafiri zaidi ya kilometa 7 hadi Hospitali ya Misheni Nyangao kufuata huduma ya X-ray. Hali hiyo ilikuwa ikiongeza gharama za matibabu kwa wagonjwa.


Sasa kilio hicho kinakwenda kuwa historia baada ya Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026 kuweka jiwe la msingi la ujenzi wa jengo la Mionzi (X-ray) katika Kituo cha Afya Mtama, Wilaya ya Mtama Mkoani Lindi.

Baadhi ya wananchi akiwemo mwajuma Saidi na Juma Mbemenya walisema kuwepo kwa huduma hiyo kwenye kituo hicho licha ya kuwapunguzia gharama ya matibabu pia itawarahisishia kupata huduma Kwa uharaka zaidi .

Akisoma taarifa ya mradi mbele ya Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Ndugu Wazo Mwang’onda, Kaimu Mganga Mkuu wa Halmashauri ya Mtama amesema mradi huo ulianza tarehe 30 Machi 2026 ukiwa ni mwendelezo wa maboresho ya huduma za afya kwa wananchi wa Tarafa ya Mtama na vitongoji vyake.

Kwa mujibu wa taarifa hiyo, mradi unakadiriwa kugharimu takriban Sh. Milioni 95 hadi kukamilika. Ambapo  mradi unatarajia kuwafikia wananchi zaidi ya 18,476 wa Tarafa ya Mtama na vijiji jirani vya Halmashauri ya Wilaya ya Tandahimba.

Akizungumza mara baada ya kuweka jiwe la msingi, Kiongozi wa Mbio za Mwenge wa Uhuru Kitaifa 2026, Wazo Mwang’onda, ameipongeza Serikali ya Awamu ya Sita chini ya Rais Dkt. Samia Suluhu Hassan kwa kuendelea kutenga fedha kuboresha miundombinu ya afya vijijini.

Aidha, ameipongeza Halmashauri ya Wilaya ya Mtama kwa kusimamia vizuri mapato ya ndani na kuyelekeza kwenye miradi yenye tija kwa jamii.

Sponsored ads

Mid 1

Mid2

Ad3