WITO WATOLEWA KUIMARISHA MATUMIZI YA TEKNOLOJIA YA VINASABA NCHINI
Apr 24, 2026
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WATAALAMU wa sekta ya afya na sayansi nchini wametakiwa kutumia majukwaa ya kitaaluma kujadili kwa kina namna ya kuimarisha matumizi ya teknolojia ya vinasaba, ili kuboresha huduma za afya na mfumo wa haki jinai.
Wito huo umetolewa na Naibu Waziri wa Afya, Dkt. Florence Samizi, alipomwakilisha Waziri wa Afya katika ufunguzi wa mkutano wa kisayansi wa teknolojia ya vinasaba uliofanyika jijini Dodoma, ukiwakutanisha wataalamu takribani 400 kutoka sekta mbalimbali.
Amesema teknolojia ya vinasaba ni nguzo muhimu katika utoaji wa huduma za kitabibu zenye ubora unaokubalika kitaifa na kimataifa, ikichangia kwa kiasi kikubwa katika upandikizaji wa viungo kama figo na uroto wa mifupa, pamoja na utambuzi wa magonjwa na tiba za kisasa zikiwemo tiba jeni na utengenezaji wa chanjo.
Aidha, amesema teknolojia hiyo imeendelea kusaidia sekta ya haki jinai kwa kuwezesha upatikanaji wa ushahidi wa kisayansi katika uchunguzi wa makosa mbalimbali, hali inayochangia kuimarisha utoaji wa haki.
Ameeleza kuwa serikali imefanya uwekezaji mkubwa katika kuimarisha miundombinu, vifaa na rasilimali watu kupitia Mamlaka ya Maabara ya Mkemia Mkuu wa Serikali, ili kuhakikisha matumizi bora ya teknolojia hiyo.
Amebainisha kuwa ujenzi wa jengo la Ofisi na Maabara ya vinasaba vya binadamu unaendele
a kwa gharama ya shilingi bilioni 16.73, sambamba na ununuzi wa mitambo ya kisasa ya uchunguzi wa vinasaba yenye thamani ya shilingi bilioni 3.5.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto zikiwemo matumizi madogo ya teknolojia hiyo katika uchunguzi wa magonjwa ya kurithi na adimu, pamoja na matumizi hafifu ya tiba binafsishi na tiba jeni.
Pia amesisitiza umuhimu wa wataalamu kuzingatia sheria na kanuni, akionya dhidi ya vitendo vya kuchukua sampuli za vinasaba na kuzisafirisha nje ya nchi bila kufuata taratibu, hali inayoweza kuhatarisha usalama wa taarifa za Watanzania.
Kwa ujumla, amewataka wadau kuibua mapendekezo yatakayosaidia serikali kuboresha zaidi sekta ya teknolojia ya vinasaba nchini.





