WANANCHI KIGOMA WAHIMIZWA KUUNGANISHA UMEME KWENYE MAENEO YAO
Mwenyekiti bodi ya ETDCO Mhandisi Raymond Mbilinyi
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
WANANCHI mkoani Kigoma wametakiwa kuunganisha umeme kwenye nyumba zao na sehemu za kiuchumi na biashara ili kuunga mkono mpango mkakati wa serikali kupeleka umeme vijiji kuwezesha shughuli za uchumi na biashara kuwana tija kubwa katika kuondoa umasikini.
Mwenyekiti wa bodi ya Wakurugenzi ya Kampuni Tanzu ya TANESCO inayojishughulisha na ujenzi, ukarabati, na uwekaji wa miundombinu ya kusafirisha na kusambaza umeme (ETDCO),Mhandisi Raymond Mbilinyi alisema hayo wakati akiongoza wajumbe na viongozi wa kampuni hiyo kukagua utekelezaji wa mradi wa kupeleka umeme vijijini mkoani Kigoma.
Mhandisi Mbilinyi alisema kuwa umeme una mchango mkubwa katika kuinua shughuli za uchumi na biashara za wananchi vijijini na ndiyo maana serikali kupitia wakala wa umeme vijijini (REA) imeamua kugharamia upelekaji umeme huo vijijini na wananchi kutakiwa kuchangia shilingi 27,000 ili kuingiza umeme kwenye maeneo yao.
Awali Kaimu Meneja Mkuu wa kampuni ya ETDCO Kampuni Tanzu ya TANESCO inayotekeleza mradi wa umeme vijijini mkoa Kigoma,Mhandisi Richard Mwanja alisema kuwa hadi sasa jumla ya kaya 1800 zimeshaunganishiwa umeme kati ya kaya 2200 zilizopangwa kufikishiwa umeme vijijini kwa ajili ya matumizi ya majumbani katika mkoa Kigoma ambapo kiasi cha shilingi Bilioni 10.5 zinatarajia kutumika kwenye utekelezaji wa mradi huo unaotarajiwa kukamilika mwezi Juni mwaka huu.
Meneja huyo alibainisha kuwa wateja wakubwa wanaotumia umeme wa viwandani 22 wameunganishiwa umeme kati ya lengo la wateja 55 huku transforma 51 zikiwa zimefungwa kati ya lengo la kufunga transforma 59 huku kasi ya wateja wa majumbani kuunganishwa umeme ikiwa ndogo licha ya Zaidi ya asilimia 90 ya miundo mbinu ya umeme kufikishwa kwenye maeneo ya wananchi.
Kwa upande wake Mwenyekiti wa kijiji cha Kaseke wilaya ya Kigoma mkoani Kigoma, Angalienni Phares ameishukuru serikali ya Rais Samia kwa kuwezesha umeme kufika vijijini na kila mwananchi kuweka umeme kwa gharama nafuu jambo ambalo litachochea sbuguli za uchumi na uzalishaji vijijini.



