WANANCHI DODOMA KUNUFAIKA NA HUDUMA ZA KISHERIA BURE
Na Hamida Ramadhan,Matukio Daima Media Dodoma
WANANCHI wa Dodoma wanatarajiwa kunufaika na huduma mbalimbali za msaada wa kisheria zitakazotolewa bure kuanzia Mei 1 hadi 15, 2026 kupitia awamu ya pili ya Kampeni ya Msaada wa Kisheria ya Mama Samia.
Huduma hizo zitahusisha ushauri wa kisheria, uwakilishi katika vyombo vya utoaji haki, uandaaji wa nyaraka pamoja na elimu ya sheria kwa jamii, zikilenga kurahisisha upatikanaji wa haki hasa kwa makundi yenye uhitaji maalum.
Akitoa taarifa hiyo Aprili 29, 2026, Mkuu wa Mkoa wa Dodoma, Rosemary Senyamule, alisema kampeni hiyo inalenga kuwafikia wananchi wengi zaidi wakiwemo wanawake, watoto, wazee, vijana na watu wenye ulemavu.
Alisema mpango huo ni sehemu ya juhudi za serikali inayoongozwa na Samia Suluhu Hassan za kusogeza huduma za haki karibu na wananchi bila gharama.
Kwa mujibu wa takwimu za awamu ya kwanza iliyofanyika mwaka 2023, zaidi ya wananchi 86,000 walipatiwa huduma hizo, huku mamia ya migogoro ikishughulikiwa na sehemu kubwa kutatuliwa.
Katika kampeni ya mwaka huu, huduma zitatolewa kuanzia ngazi ya wilaya hadi vijiji na mitaa, pamoja na kufanyika katika maeneo yenye mikusanyiko mikubwa ya watu ili kuwafikia wananchi wengi kwa wakati mmoja.
Aidha, wananchi watapata huduma za usajili wa vyeti vya kuzaliwa na vifo kupitia Wakala wa Usajili, Ufilisi na Udhamini (RITA) pamoja na elimu ya utatuzi wa migogoro kwa njia mbadala.
Mkuu huyo wa mkoa amehimiza wananchi kujitokeza kwa wingi kutumia fursa hiyo, akisisitiza kuwa upatikanaji wa haki ni msingi muhimu wa maendeleo ya jamii.
Kauli mbiu ya kampeni hiyo ni “Msaada wa Kisheria kwa Haki, Usawa, Amani na Maendeleo.”
MWISHO.
