WANANCHI BUKOBA WALALAMIKIA KUPANDA KWA BEI YA NYAMA
Na Anold Deogratias Matukio Daima News Kagera
Kufuatia kupanda kwa bei ya Nyama mjini Bukoba mkoani Kagera kutoka shilingi elfu kumi hadi elfu kumi na mbili imewatia hofu wakazi wa mji huo juu ya utumiaji wa kitoweo hicho muhimu hasa nyakati hizi za sikukuu za pasaka.
Wakizungumza na waandishi wa habari akiwemo Robert Katunzi amesema kuwa kupanda kwa bei hiyo itawaathiri wananchi na itasababisha kupungua kwa matumizi ya kitoweo hicho hasa siku za sikukuu kutokana na kipato cha wananchi walio wengi kuwa chini.
“kupanda kwa bei ya nyama itasababisha matumizi ya nyama yatapungua mtu aliyekuwa amepanga kununua kilo mbili au moja sasa atanunua nusu kilo hasa msimu huu wa sikukuu za pasaka, kiwango hiki cha shilingi elfu mbili ni kikubwa kwa mwananchi wa kawaida”
Naye Erasto Kajuna amesema kuwa kupanda kwa bei ya nyama inawezekana imesababishwa na kupanda kwa bei ya mafuta hivyo amewaomba wawakilishi wao bungeni kuwatetea wananchi ili kupunguza bei ya mafuta ili kuwezesha kupungua kwa bei za bidhaa nyingine kama nyama.
“ng’ombe wamepungua ndio maana bei ya nyama imepanda ng’ombe ni wachache huko mnanadani na sio kwamba tumepandisha bei ili kuwakomoa wananchi, wafanyabiashara wamepandisha kidogo ili na wao wapate faida tuwaombe wananchi watuvumilie kwa hali hii”
Hata hivyo aliyewai kuwa msimamizi wa ranchi za taifa mkoani Kagera Mashaka Omary ameleeza kuwa kwa sasa ni kipindi cha upungufu wa mifugo kutokana na wafugaji kuwa kwenye uzalishaji wa mifugo na sio kipindi cha uuzaji wa mifugo.
“kipindi hiki kinaangukia katika msimu wa uzalishaji wa mifugo hali inayosababisha kupungua kwa mifugo minadani na kusababisha kupanda kwa bei ya nyama lakini ni kipindi cha muda kuanzia mwezi wa sita kitakuwa ni kipindi cha uuzaji wa mifugo hivyo bei itashuka tena”
Katika mji wa Bukoba mkoani Kagera kuanzia April 2, 2026 bei ya Nyama imepanda kutoka shilingi elfu kumi ya awali hadi shilingi elfu kumi na mbilia.


