CCM MBOZI YATAKA KUIMARISHWA KWA USIMAMIZI WA MIRADI YA MAENDELEO
Apr 2, 2026
Na Moses Ng’wat, Mbozi.
KAMATI ya Siasa ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Wilaya ya Mbozi imeridhishwa na utekelezaji wa miradi mbalimbali ya maendeleo inayotekelezwa wilayani humo, huku ikitaka kuimarishwa zaidi kwa usimamizi ili kudhibiti kasoro ndogo ndogo.
Kauli hiyo ilitolewa Aprili 1, 2026 na Mwenyekiti wa CCM Wilaya ya Mbozi, Majaliwa Mlawizi, kwa niaba ya wajumbe wa kamati hiyo, wakati wa ziara ya kukagua miradi ya maendeleo katika Jimbo la Mbozi, chini ya Halmashauri ya Wilaya hiyo.
Akizungumza baada ya kukagua mradi wa ujenzi wa vyumba viwili vya maabara katika Shule ya Sekondari Msanyila, Mlawizi alisema kamati imeridhishwa na hatua iliyofikiwa na kusisitiza umuhimu wa kuendelea kusimamia miradi hiyo kwa umakini zaidi ili kuhakikisha inakamilika kwa ubora unaotakiwa.
Aidha, aliwapongeza watendaji wa Halmashauri ya Wilaya ya Mbozi pamoja na Ofisi ya Mkuu wa Wilaya, chini ya Mkuu wa Wilaya, Hamad Mbega, kwa usimamizi mzuri wa miradi inayotekelezwa kwa fedha kutoka Serikali Kuu.
Kwa mujibu wa taarifa ya Halmashauri, Shule ya Sekondari Msanyila ilipokea shilingi milioni 60 mwezi Agosti 2025 kwa ajili ya ukamilishaji wa vyumba hivyo vya maabara. Hata hivyo, hadi sasa jumla ya shilingi 63,768,262 zimetolewa, ambapo shilingi 40,072,036 tayari zimetumika katika utekelezaji wa mradi huo.
Pamoja na kuridhishwa na maendeleo hayo, kamati ilisisitiza haja ya kuongeza umakini katika usimamizi wa miradi ili kudhibiti kasoro ndogondogo zinazoweza kujitokeza wakati wa utekelezaji.
Katika ziara hiyo, kamati pia ilitembelea miradi mingine ikiwemo ujenzi wa Shule Mpya ya Sakamwela, ujenzi wa madarasa na matundu ya vyoo katika Shule ya Msingi Ivwanga, ukamilishaji wa bwalo katika Shule ya Sekondari Kisimani, pamoja na mradi wa maji wa Hatelele uliopo Kata ya Shiwinga.
Kamati ilihimiza kuendelea kwa ushirikiano kati ya viongozi, wataalamu na wananchi ili kuhakikisha miradi hiyo inaleta tija iliyokusudiwa na kuchochea maendeleo endelevu ya Wilaya ya Mbozi.



