WADHIBITI UBORA WAAGIZWA KUSIMAMIA CHAKULA SHULENI KWA UMAKINI
Apr 20, 2026
Na Hamida Ramadhan, Matukio Daima Media Dodoma
WADHIBITI ubora wa elimu nchini wametakiwa kuongeza umakini katika kusimamia chakula kinachotolewa mashuleni ili kulinda afya za wanafunzi na kuimarisha ufaulu wao darasani.
Agizo hilo limetolewa na Kamishna wa Elimu, Dk Lyabwene Mtahabwa jijini Dodoma huku akisisitiza kuwa, chakula kisicho na ubora kinaweza kusababisha madhara ya kiafya kwa wanafunzi.
Amesema ni jukumu la wadhibiti ubora katika halmashauri zote kuhakikisha vyakula vinavyoandaliwa na vinavyouzwa shuleni vinakidhi viwango vinavyotakiwa.
Dk Mtahabwa ameonya kuwa baadhi ya vyakula vinavyopatikana mashuleni havina uhakika wa usalama wake na vinaweza kuathiri afya za watoto.
Ametaja madhara yanayoweza kujitokeza kuwa ni pamoja na matatizo ya kiafya kama viriba tumbo vinavyotokana na ulaji usiofaa.
Ameagiza kufanyika kwa ufuatiliaji wa karibu katika shule zote ili kubaini aina ya vyakula vinavyotolewa kwa wanafunzi.
“Tusimkubali kwa vyovyote anayechezea afya za watoto wetu,” amesema Dk Mtahabwa.
Ameongeza kuwa ni muhimu kwa wadau wote wa elimu kushirikiana katika kuhakikisha chakula kinachotolewa mashuleni ni salama.
Dk Mtahabwa amesisitiza kuwa lishe bora ni msingi wa mafanikio ya mchakato wa ufundishaji na ujifunzaji.
Kwa upande wake, Mkurugenzi Mkazi wa SwissAid Tanzania, Betty Malaki, amesema mradi wa CRISP unalenga kuboresha mifumo ya ununuzi wa chakula mashuleni.
Amesema mradi huo utasaidia kuhakikisha wanafunzi wanapata lishe bora na salama bila madhara ya kiafya.
Naye Ofisa Programu wa Sera kutoka World Food Programme, Abiud Gamba, amesema lishe shuleni ina mchango mkubwa katika kuongeza mahudhurio na umakini wa wanafunzi.
Ameeleza kuwa ushahidi unaonyesha kuwa programu za lishe shuleni huleta matokeo chanya katika elimu na uchumi.
Hata hivyo, amesema bado kuna changamoto ya upatikanaji wa lishe kamili mashuleni, hususan vyakula vya protini, mboga na matunda.



