KILUMBE NG'ENDA AWAFUNDA VIONGOZI CCM
Na Fadhili Abdallah,Kigoma
NAIBU Katibu Mkuu Taifa wa Jumuia ya Wazazi ya Chama Cha Mapinduzi (CCM) Kilumbe Ng’enda amewataka watendaji na viongozi wa jumuia hiyo kuifanya jumuia hiyo kuwa chuo cha malezi na tabia njema ili kuendelea kutoa viongozi wenye maadili na wanaozingatia maslahi ya umma.
Ng’enda alisema hayo mjini Kigoma juzi usiku wakati wa hafla ya kumuaga aliyekuwa Katibu wa jumuia ya wazazi mkoa Kigoma, Abushekhe Kodema ambaye amestaafu utumishi ndani ya jumuia hiyo na kusema kuwa kitendo cha mtumishi kustaafu na kuagwa na watumishi na viongozi wenzake ni heshima kubwa kwa mtumishi huyo.
Naibu Katibu Mkuu huyo alisema kuwa hiyo inaonyesha kuwa kiongozi huyo alikuwa sehemu ya maisha ya watumishi na viongozi wenzake kutokana na kuzingatia maadili, nidhamu, uadilifu na maslahi ya umma badala ya kuangalia maslahi yake na hivyo kutaka viongozi na watendaji wa Jumuia hiyo kufuata misingi hiyo.
Akizungumza katika hafla hiyo, Katibu huyo Mstaafu wa Jumuia ya wazazi mkoa Kigoma, Abushekhe Kodema ameshukuru viongozi na watendaji wenzake kwa kumuandalia sherehe hiyo ya kumuaga na kumpa zawadi mbalimbali ambazo zitakuwa za kukumbukwa kwenye utumishi wake.
Hata hivyo Mtumishi huyo mstaafu alilazimika kutokwa na machozi wakati akipokea tuzo ya utumishi uliotukuka akieleza kuwa alikuwa akitimiza majukumu yake kwa mujibu wa taratibu za kazi na kwambaa tuzo hiyo itakuwa somo na fundisho kubwa katika maisha yake.
